Mwanamke wa Uganda mwenye umri wa miaka 70 ajifungua mapacha

Bi Namukwaya alisema kwamba ujauzito wake umekuwa mgumu kwani mpenzi wake alimtelekeza alipogundua kuwa angezaa mapacha.

Muhtasari

• Safina Namukwaya alijifungua mvulana na msichana kwa njia ya upasuaji katika kituo cha uzazi katika mji mkuu, Kampala.

• "Tumefanikiwa ajabu - kujifungua mapacha kwa mama mzee zaidi barani Afrika mwenye umri wa miaka 70!" 

Safina mwanamke wa Uganda aliyejifungua mapacha kwa umri wa miaka 70
Safina mwanamke wa Uganda aliyejifungua mapacha kwa umri wa miaka 70
Image: HISANI

Mwanamke mwenye umri wa miaka 70 amejifungua watoto mapacha kufuatia matibabu ya IVF,kwa mujibu wa hospitali moja nchini Uganda.

Safina Namukwaya alijifungua mvulana na msichana kwa njia ya upasuaji katika hospitali moja mjini Kampala.

Bi Namukwaya, ambaye ni mmoja wa wanawake wazee zaidi kuzaa, aliambia vyombo vya habari kuwa ni "muujiza".

Hospitali ilimpongeza, ikisema ni zaidi ya "mafanikio ya matibabu; ni juu ya nguvu na uthabiti wa roho ya mwanadamu".

"Tumefanikiwa ajabu - kujifungua mapacha kwa mama mzee zaidi barani Afrika mwenye umri wa miaka 70!" Kituo cha Kimataifa cha Hospitali ya Wanawake na Uzazi kilisema.

Ilisema alikuwa amejifungua watoto siku ya Jumatano baada tu ya adhuhuri, na kusema kuwa mama na watoto wote wako salama.

Bi Namukwaya alisema  kwamba ujauzito wake umekuwa mgumu kwani mpenzi wake alimtelekeza alipogundua kuwa angezaa mapacha.

“Wanaume hawapendi kuambiwa kuwa umebeba zaidi ya mtoto mmoja, tangu nilipolazwa hapa mume wangu hajawahi kufika,” alisema.

Hii ni mara ya pili kwa Bi Namukwaya kujifungua katika kipindi cha miaka mitatu. Alijifungua mtoto wa kike mnamo 2020.

Alisema alitamani kupata watoto baada ya kudhihakiwa kwa kukosa mtoto.

"Niliwachunga watoto wa watu na kuwaona wakikuwa na kuniacha peke yangu. Nilijiuliza ni nani atanitunza nikizeeka," alinukuliwa akisema.

Haijabainika iwapo alitumia yai la wafadhili au lile lake ambalo liligandishwa na kuhifadhiwa alipokuwa mdogo.

Kwa kawaida wanawake hupitia kipindi cha kukoma hedhi kati ya umri wa miaka 45 na 55. Uzazi hupungua wakati huu lakini maendeleo ya dawa yamewawezesha kujifungua.

Urutubishaji katika vitro (IVF) ni mojawapo ya mbinu kadhaa. Wakati wa mchakato huo yai hutolewa kutoka kwa ovari ya mwanamke na kurutubishwa na manii kwenye maabara.

Yai lililorutubishwa, linaloitwa kiinitete, kisha huwekwa ndani ya tumbo la uzazi la mwanamke ili kukua.