Ghadhabu ya Wakenya Serikali ikiongeza ada za malipo kwa matumizi ya Nairobi Expressway

Waziri Murkomen alijitokeza na kutetea ada hizo mpya akisema kwamba ilibidi ziongezwe kutokana na mabadiliko katika soko na pia kuporomoka kwa shilingi ya Kenya dhidi ya dola ya Kimarekani.

Muhtasari

• Katika njia hiyo hiyo, magari yanayotoka katika kituo cha Capital Hill na Haile Selassie yatalipa Ksh.410 kutoka Ksh.210.

• Toka katika Museum Hill, The Mall na kituo cha Nairobi Westland kitavutia kiwango cha Ksh.500 kutoka Ksh.310.

Barabara kuu ya Expressway jijini Nairobi, Kenya
Barabara kuu ya Expressway jijini Nairobi, Kenya
Image: The Star//Maktaba

Wakenya wa matabaka mablimbali haswa wale wanaotumia barabara ya kisasa ya Expressway jijini Nairobi wameonesha kughadhabishwa kwao na serikali baada ya ada mpya za matumizi ya barabara hiyo kuchapishwa kwenye gazeti rasmi la serikali.

Waziri wa miundombinu na barabara Kipchumba Murkomen alitangaza ada hizo mpya katika gazeti la serikali mnamo Desemba 31 na kusema kwamba ada mpya za malipo zitaanza kufanya kazi mara moja.

Katika viwango hivyo vipya, waendeshaji magari wanaoingia kwenye Barabara ya Express ya Mlolongo na kutoka katika kituo cha SGR na Eastern ByPass watalazimika kulipa Ksh.250 kutoka Ksh.100 ya sasa, huku wale wanaotoka katika Barabara ya Southern ByPass watalipa Ksh.330 hadi kutoka Ksh.210.

Katika njia hiyo hiyo, magari yanayotoka katika kituo cha Capital Hill na Haile Selassie yatalipa Ksh.410 kutoka Ksh.210.

Toka katika Museum Hill, The Mall na kituo cha Nairobi Westland kitavutia kiwango cha Ksh.500 kutoka Ksh.310.

Viwango hivyo pia vitatumika kwa madereva wanaosafiri kupitia njia iliyo kinyume kutoka kituo cha kuingilia cha Nairobi Westlands hadi kituo cha kutokea cha Mlolongo.

Njia fupi kutoka Syokimau hadi kituo cha SGR na zile za SGR na kituo cha JKIA hadi Eastern Bypass zitagharimu madereva Ksh.170 kutoka Ksh.100.

Ada hizi mpya zilivutia kero kutoka kwa baadhi ya Wakenya katika mtandao wa X, awali ukijulikana kama Twitter.

Hata hivyo, waziri huyo alijitokeza na kutetea ada hizo mpya akisema kwamba ilibidi ziongezwe kutokana na mabadiliko katika soko na pia kuporomoka kwa shilingi ya Kenya dhidi ya dola ya Kimarekani.

“Ukichukua kiwango cha juu ambacho ni kutoka 360 hadi 500 utapata tofauti ya Shilingi 140. ukigawanya Kshs 140 kwa Kshs 360 na kuzidisha kwa 100 utapata 38.89%. Sasa marekebisho ya mwisho yalifanyika wakati dola moja ilikuwa sawa na Kshs 113.14. Sasa dola ni Ksh 157 na kwa kutumia njia sawa yaani 157 minus 113 ambayo ni sawa na 44. Gawanya 44 kwa 113 na zidisha kwa 100 na utapata 38.9 %. Hivyo ongezeko ni sawia,” aliandika.