Tumia barabara mbadala - CS Murkomen kwa wanaolalamika kuhusu ada mpya za Expressway

Katika viwango hivyo vipya, waendeshaji magari wanaoingia kwenye Barabara ya Express ya Mlolongo na kutoka katika kituo cha SGR na Eastern ByPass watalazimika kulipa Ksh.250 kutoka Ksh.100 ya sasa

Muhtasari

• Murkomen alisema kwamba barabara hiyo si ya kuvutia msongamano mkubwa wa magari na hivyo wanaohisi ada hizo ni za juu basi wana chaguo la kutumia barabara nyingine.

Waziri wa uchukuzi wa umma na miundombinu Kipchumba Mukromen amejitokeza na kutetea vikali ada mpya za malipo kwa ajili ya matumizi ya barabara ya kisasa ya Expressway jijini Nairobi.

Murkomen kupitia ukurasa wake wa X aliwataka wanaolalamika kwa kuhisi kudhulumiwa kwa ada hizo mpya kutumia barabara mbadala ambazo hazitozwi ada kwa ajili ya matumizi.

Hii ni baada ya Wakenya wengi kulalamika mitandaoni pindi tu baada ya ada hizo mpya kuchapishwa kwenye gazeti rasmi la serikali, ikiwa ni nyongeza ya hadi asilimia 38.9 kutoka ada za awali ambazo zimekuwa zikitekelezwa tangu uzinduzi wa barabara hiyo takribani miaka miwili iliyopita.

Murkomen alisema kwamba barabara hiyo si ya kuvutia msongamano mkubwa wa magari na hivyo wanaohisi ada hizo ni za juu basi wana chaguo la kutumia barabara nyingine.

“Jambo zuri kuhusu Express way kwanza ni kwamba serikali ya Kenya haikutoa dhamana ya ujazo wa trafiki vinginevyo mlipakodi sasa angekuwa analipa sana kutokana na riba iliyokusanywa na mfumuko wa bei pamoja na tofauti ambayo haijafikiwa na mtiririko mdogo wa trafiki. Pili, mtumiaji ana njia mbadala ambayo haitozwi ada,” Murkomen alisema.

Akirejelea ada hizo mpya, waziri huyo alieleza kwamba ililazimu ziongezwe kutokana na mfumko wa bei lakini pia shilingi ya Kenya kupoteza udhabiti dhidi ya dola ya Kimarekani.

“Ukichukua kiwango cha juu ambacho ni kutoka 360 hadi 500 utapata tofauti ya Shilingi 140. ukigawanya Kshs 140 kwa Kshs 360 na kuzidisha kwa 100 utapata 38.89%. Sasa marekebisho ya mwisho yalifanyika wakati dola moja ilikuwa sawa na Kshs 113.14. Sasa dola ni Ksh 157 na kwa kutumia njia sawa yaani 157 minus 113 ambayo ni sawa na 44. Gawanya 44 kwa 113 na zidisha kwa 100 na utapata 38.9 %. Hivyo ongezeko ni sawia,” alieleza.

Katika viwango hivyo vipya, waendeshaji magari wanaoingia kwenye Barabara ya Express ya Mlolongo na kutoka katika kituo cha SGR na Eastern ByPass watalazimika kulipa Ksh.250 kutoka Ksh.100 ya sasa, huku wale wanaotoka katika Barabara ya Southern ByPass watalipa Ksh.330 hadi kutoka Ksh.210.

Katika njia hiyo hiyo, magari yanayotoka katika kituo cha Capital Hill na Haile Selassie yatalipa Ksh.410 kutoka Ksh.210.

Toka katika Museum Hill, The Mall na kituo cha Nairobi Westland kitavutia kiwango cha Ksh.500 kutoka Ksh.310.

Viwango hivyo pia vitatumika kwa madereva wanaosafiri kupitia njia iliyo kinyume kutoka kituo cha kuingilia cha Nairobi Westlands hadi kituo cha kutokea cha Mlolongo.

Njia fupi kutoka Syokimau hadi kituo cha SGR na zile za SGR na kituo cha JKIA hadi Eastern Bypass zitagharimu madereva Ksh.170 kutoka Ksh.100