Mtahiniwa wa kike wa KCPE apatwa na mshangao kuitwa shule ya upili ya wavulana

Alikuwa amechagua shule kadhaa katika kitengo cha Shule za Kitaifa, zikiwemo Alliance, Starehe Girls na Kisumu Girls lakini akapokezwa barua ya kujiunga na shule ya wavulana ya Lenana.

Muhtasari

• Kweli alijipatia nafasi katika shule ya upili ya kitaifa, lakini dosari likawa kwamba shule hiyo ni ya wavulana pekee hali ya kuwa yeye ni msichana.

Watahiniwa wa darasa la nane wakalia mtihani wa KCPE
Watahiniwa wa darasa la nane wakalia mtihani wa KCPE
Image: MAKTABA

Biwi la mshangao liligubika familia moja katika kaunti ya Siaya baada ya mtoto wao wa kike aliyefanya vizuri katika mtohani wa kitaifa wa darasa la nane KCPE kuitwa katika shule ya kitaifa ya wavulana.

Gloria Owino alifanya vizuri kutoka shule ya msingi ya Nyalgunga na kupata alama 389, ha hivyo kuhitimu kujiunga shule ya upili ya kitaifa.

Kweli alijipatia nafasi katika shule ya upili ya kitaifa, lakini dosari likawa kwamba shule hiyo ni ya wavulana pekee hali ya kuwa yeye ni msichana.

Gloria, ambaye alizungumza na kituo kimoja cha redio humu nchini katika nyumba ya wazazi wake katika kituo cha biashara cha Nyalgunga, anasema alipata nafasi katika Shule ya Lenana, ambayo ni shule ya wavulana.

Mwanafunzi huyo ambaye sasa amekwama anadai kuwa alijaribu bila mafanikio kusubiri barua nyingine ya kuitwa kwa sababu alikuwa amechagua shule kadhaa katika kitengo cha Shule za Kitaifa, zikiwemo Alliance, Starehe Girls na Kisumu Girls.

Wanafunzi waliofanya mitihani ya KCPE wanatarajiwa kuanza kujiunga na kidato cha kwanza kuanzia Januari 15 ambayo ni wiki kesho na ndoto ya mwanafunzi huyo bado ipo katika hatihati kwani bado hajapata barua nyingine.