Kampuni za Airtel na Telkom zapewa onyo na mamlaka ya mawasiliano kuhusu huduma duni

“Mamlaka ya Mawasiliano ya Kenya (CA) imetoa notisi kwa Airtel na Telkom Kenya kwa kutozingatia ubora wa huduma (QoS) zinazotolewa kwa watumiaji kwenye mitandao yao ya simu." CA ilisema.

Muhtasari

• CA inasema kwamba kampuni ya simu inakadiriwa kuwa inakidhi mahitaji inapofikia asilimia 80 ya seti za QoS KPIs.

WI-FI
WI-FI
Image: HISANI

Mamlaka inayosimamia mawasiliano nchini Kenya, CA imetoa onyo kali kwa kampuni za mawasiliano za Telkom na Airtel kuhusu kile kinachotajwa kuwa ni huduma duni kwa wateja.

Kwa mujibu wa ripoti iliyochapishwa kwenye Business Daily, kampuni hizo mbili zilipewa notisi kuhusu kutozingatia masharti ya utendakazi ya hakikisho la huduma bora (QoS) kwa wateja.

Katika ripoti yake ya hivi punde ya QoS ya mwaka uliomalizika Juni 2023, mdhibiti wa sekta hiyo anaonyesha kuwa ni kiongozi wa soko pekee Safaricom aliyevuka kiwango cha utendakazi cha asilimia 80 baada ya kuchapisha alama 90 za seti za Viashiria Muhimu vya Utendakazi (KPIs).

“Mamlaka ya Mawasiliano ya Kenya (CA) imetoa notisi kwa Airtel na Telkom Kenya kwa kutozingatia ubora wa huduma (QoS) zinazotolewa kwa watumiaji kwenye mitandao yao ya simu za rununu,” mdhibiti alisema kwenye taarifa kama ilivyonukuliwa na Business Daily.

Kulingana na ripoti hiyo, Airtel na Telkom Kenya zilipata asilimia 79 na asilimia 65 mtawalia, ikiwa ni wastani wa sekta ya asilimia 72.4, na alama hiyo ikiwa imeshuka kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na wastani wa asilimia 82.3 iliyofikiwa mwaka hadi Juni 2022 na asilimia 75.5. katika mwaka uliopita.

CA inasema kwamba kampuni ya simu inakadiriwa kuwa inakidhi mahitaji inapofikia asilimia 80 ya seti za QoS KPIs.

“Mitandao ya Airtel Kenya na Telkom Kenya ilishindwa kufikia sio tu shabaha zao za mawasiliano bali pia idadi ya KPI muhimu zaidi za QoS, hasa 'Uwiano wa Simu Usiofanikiwa' na 'Data Internet' KPIs, ambayo ni kiashirio cha ufikiaji na upatikanaji wa Intaneti/ upatikanaji mtawalia,” inasomeka ripoti hiyo.