Kisumu: Mama Margaret Kenyatta ahudhuria ibada ya kumbukumbu ya babake Raila Odinga

Kiongozi wa Azimio Raila Odinga ambaye ni mtoto wa Jaramogi alipanga ibada ya ukumbusho kusherehekea na kuheshimu urithi wake na nafasi yake katika historia ya Kenya.

Muhtasari

• Mzee Jaramogi alifariki Januari 20, 1994 huko Kisumu.

• Ibada hiyo ilifanyika katika Kanisa la St. Stephen's Cathedral mjini Kisumu.

Mama Margaret Kenyatta miongoni mwa watu waliohudhuria ibada ya kumbukumbu ya Jaramogi
Mama Margaret Kenyatta miongoni mwa watu waliohudhuria ibada ya kumbukumbu ya Jaramogi
Image: HISANI

Aliyekuwa Mkewe Rais Margaret Kenyatta siku ya Jumamosi alihudhuria ibada ya kumbukumbu ya marehemu Mzee Jaramogi Oginga Odinga.

Mzee Jaramogi alifariki Januari 20, 1994 huko Kisumu.

Ibada hiyo ilifanyika katika Kanisa la St. Stephen's Cathedral mjini Kisumu.

Margaret alionekana akiwa ameketi kando ya Gavana wa Siaya James Orengo wakati wa ibada.

Viongozi hao walikuwa wameketi mstari wa mbele wakifuatilia ibada ya kumbukumbu.

Kiongozi wa Azimio Raila Odinga ambaye ni mtoto wa Jaramogi alipanga ibada ya ukumbusho kusherehekea na kuheshimu urithi wake na nafasi yake katika historia ya Kenya.

Raila aliwaalika wasomi mashuhuri, wana-Pan-Africanists, viongozi wa fikra na wanahabari kuzungumza kwenye hafla hiyo.

Siku hii inaadhimisha miaka 30 tangu Makamu wa Rais mwanzilishi wa taifa hilo kufariki.

Jaramogi Ajuma Oginga Odinga alikuwa mwanasiasa mashuhuri na mmoja wa viongozi wa wapigania uhuru wa Kenya waliosaidia kupata uhuru wa nchi hiyo.

Alizaliwa mnamo Oktoba 1911.

Aliteuliwa kuwa waziri wa mambo ya ndani mwaka wa 1963, na mwaka wa 1964 akawa makamu wa rais chini ya mwanzilishi wa baba Mzee Jomo Kenyatta.

Mkosoaji mkali wa Kenyatta, Jaramogi alihudumu kama Makamu wa Rais kuanzia Desemba 12, 1964, hadi Aprili 14, 1966, alipojiuzulu na alibaki kiongozi wa upinzani mkali hadi kifo chake.