Toa njia mbadala kwa mipango yangu na sio maandamano - Ruto kwa upinzani

“Waliniambia nisifanye mpango wa nyumba, kazi za kidigitali na nyinginezo, nikawauliza mpango wao wakasema wanaandaa maandamano, maandamano yatatengeneza ajira?" Ruto aliuliza.

Muhtasari

• Rais aliongeza kuwa serikali ya Kenya Kwanza inapanga kubuni ajira kupitia makazi, kazi za kidijitali, vituo vya ICT

• Ruto aliwataka vijana hao kuchukua fursa ya kazi zilizotangazwa serikalini na kutuma maombi.

• Rais mara kadhaa amewahimiza Wakenya kukumbatia mipango ya serikali ambayo italeta ajira.

RUTO WILLIAM
RUTO WILLIAM
Image: PCS

Rais William Ruto ameuambia Upinzani kukoma kupiga vita mipango yake ya maendeleo na badala yake wape njia mbadala za mipango ya serikali.

Akizungumza Jumapili wakati wa ibada ya maombi ya madhehebu mbalimbali mjini Busia, Rais alisema kuandaa maandamano hakutasaidia vijana kupata ajira.

“Waliniambia nisifanye mpango wa nyumba, kazi za kidigitali na nyinginezo, nikawauliza mpango wao wakasema wanaandaa maandamano, maandamano yatatengeneza ajira?

"Wale wa Upinzani wakome kushawishi Wakenya kwa maandamano na badala yake watupe mpango wao mbadala wa kubuni nafasi za kazi kwa mamilioni ya Wakenya."

Rais aliongeza kuwa serikali ya Kenya Kwanza inapanga kubuni ajira kupitia makazi, kazi za kidijitali, vituo vya ICT, usafirishaji wa wafanyikazi na kilimo ili kuunda nafasi za kazi.

"Mpango wao mbadala ni upi? Hilo ndilo swali kubwa."

Ruto aliwataka vijana hao kuchukua fursa ya kazi zilizotangazwa serikalini na kutuma maombi.

Rais mara kadhaa amewahimiza Wakenya kukumbatia mipango ya serikali ambayo italeta ajira.

Rais alisema kuna haja ya hatua za haraka, za makusudi na za kimkakati za kukabiliana na ukosefu wa ajira nchini.

Alisema Serikali imebaini Mpango wa Nyumba za bei nafuu, ajira za kidijitali na usafirishaji wa vibarua kuwa ni baadhi ya programu zitakazotumiwa kutengeneza ajira.

"Isipokuwa tutafanya kazi kimakusudi katika programu zinazounda nafasi za kazi, tutaendelea kuwa na mamilioni ya vijana wetu mitaani bila kazi huku mzozo wa ukosefu wa ajira ukiongezeka," alisema Jumatano alipokuwa akizungumza huko Kitale.

Rais alibainisha kuwa serikali inaanzisha vituo vya TEHAMA katika kila wadi ili kuwapa vijana ujuzi wa kidijitali ili kupata fursa za mtandaoni.

Alisema vituo vya kidijitali tayari vimewezesha vijana 119,000 kupata kazi za kidijitali.

“Tunawaomba wale ambao wamepitia mafunzo katika vituo hivi wawaelekeze wengine ili tuweze kuwafikia vijana wengi iwezekanavyo,” alisema.