5 wafariki katika ajali iliyohusisha wanawake kutoka mkutano wa maombi huko Subukia Shrine

Walioathiriwa ni pamoja na dereva na wanawake kutoka St. Peter's Gaitega, sehemu ya Parokia ya Kanisa Kuu la Jimbo Katoliki la Murang'a.

Muhtasari

• Kundi hilo lilikuwa likisafiri kwa matatu ajali hiyo ilipotokea, na watu waliojeruhiwa wamelazwa katika hospitali mbalimbali.

Crime Scene
Image: HISANI

Watu watano walipoteza maisha na wengine tisa kupata majeraha katika ajali mbaya ya barabarani eneo la Mahiga Meeru kando ya barabara ya Nyahururu-Nyeri Jumamosi jioni.

Walioathiriwa ni pamoja na dereva na wanawake kutoka St. Peter's Gaitega, sehemu ya Parokia ya Kanisa Kuu la Jimbo Katoliki la Murang'a.

Walionusurika walisimulia kwamba walikuwa wakirejea nyumbani baada ya kushiriki katika mkutano wa maombi ya Kitaifa katika Madhabahu ya Marian ya Subukia, iliyoandaliwa na Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki (CWA) Ijumaa jioni.

Kundi hilo lilikuwa likisafiri kwa matatu ajali hiyo ilipotokea, na watu waliojeruhiwa wamelazwa katika hospitali mbalimbali.

Watu watatu walionusurika walikimbizwa katika Kaunti ya Nyahururu na Hospitali ya Rufaa ambako walitibiwa, wawili kati yao waliruhusiwa huku mwingine akilazwa akiuguza majeraha kichwani, ambapo, miili ya wanne walioaga dunia papo hapo ilipelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Kaunti ya Nyahururu.

Wengine waliookolewa walipelekwa katika hospitali tofauti kaunti ya Nyeri.

Walionusurika walisema dereva wa gari la viti 14 walilokuwa wakisafiria alikuwa akijaribu kukwepa kugonga trela iliyokuwa ikitoka upande tofauti bila mafanikio.

Walisema trela hilo lilionekana kupoteza breki na kupoteza mwelekeo kabla ya kugonga gari lao.

Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Nyandarua Faith Gitau ni miongoni mwa waliosaidia manusura katika eneo la tukio.

Polisi wameanzisha uchunguzi kuhusu ajali hiyo. Tukio hili linaongeza udharura wa kampeni inayoendelea ya kukabiliana na ongezeko la idadi ya ajali nchini.

Huku hadi watu 4,000 wakipoteza maisha kila mwaka na maelfu zaidi kupata majeraha, matukio haya yana madhara makubwa kwa familia kote nchini.