Mwili wa muigizaji Charles Ouda kuchomwa Alhamisi

Ibada ya kuchoma maiti imetengwa kwa wanafamilia wa karibu pekee.

Muhtasari

•Waandalizi wa mazishi hayo walisema ibada ya kanisa itafanywa katika Kanisa la All Saints Cathedral mwendo saa nne asubuhi kisha mwil kuchomwa katika makaburi ya Kariokor.

CHARLES OUDA
CHARLES OUDA
Image: HISANI

Mwili wa marehemu muigizaji Charles Ouda almaarufu ‘Charli’ utachomwa siku ya Alhamisi, Februari 15, 2024.

Haya ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwenye kundi la WhatsApp ambapo mipango ya maziko inaratibiwa.

Waandalizi wa mazishi hayo walisema kuwa ibada ya kanisa itafanywa katika Kanisa la All Saints Cathedral siku ya Alhamisi mwendo saa nne asubuhi  na kisha mwili wa marehemu  utachomwa katika makaburi ya Kariokor.

Ibada ya kuchoma maiti imetengwa kwa wanafamilia wa karibu pekee.

Mwili wa muigizaji huyo marehemu utaondolewa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Chiromo siku ya Jumatano, Februari 14, 2024, na kupelekwa nyumbani kwa familia yake kwa maombolezi ya mkesha wa usiku kucha.

Harakati ya kuchangisha pesa za kugharamia mazishi imepangwa kufanyika siku ya Jumanne, Februari 13, saa kumi na moja unusu jioni katika chumba cha Higher Trinity katika All Saints Cathedral, Nairobi.

Waandalizi wa mazishi hayo wanatarajiwa kushiriki habari zaidi kuhusu mazishi hayo siku ya Jumatatu huku wanafamilia na marafiki wakiwa wamealikwa kwa mipango ya mazishi katika nyumba ya familia katika eneo la Loresho, Nairobi.

Familia ya marehemu Charli pia imeeleza kuthamini kwao msaada na upendo ambao wamepokea katika nyakati hizi ngumu.

Familia ya marehemu Ouda na mchumba wake Ciru Muriuki ilitangaza kufariki kwake siku ya Jumapili. Alifariki akiwa na umri wa miaka 38.

"Wapendwa marafiki na familia, ni kwa huzuni kubwa kwamba tunashiriki kifo cha Charles 'Charlie' J.Ouda usiku wa Februari 3, 2024," ilisema taarifa.

Familia iliomba kila mtu aheshimu ufaragha wao na aliyekuwa mchumba wake wanapopitia kipindi hiki kigumu.