Fahamu kwa nini mwili wa hayati Mwai Kibaki huenda ukafukuliwa

Hata hivyo, wanawe KIbaki wamepinga majaribio ya kuufukua mwili wa baba yao, wakisema kuufanyia uchunguzi wa DNA kutakiuka kanuni za maisha yao ya kibinafsi.

Muhtasari

• Wanataka kutambuliwa kama watoto wake na wanufaika wa mali yake.

•  Ocholla na JNL wanataka mahakama iamuru uchunguzi wa DNA wa ndugu au baba.

Mwili wa Mwai Kibaki
Mwili wa Mwai Kibaki
Image: ENOS TECHE//THE STAR

Huku mzozo wa mirathi ya hayati rais wa tatu wa Kenya, Mwai KIbaki ukiendelea kukita mizizi, sasa imebainika kwamba suluhu pekee na la mwisho huenda likawa ni kufukuliwa kwa maiti yake iliyozikwa mapema mwaka 2022.

Kwa mujibu wa taarifa kwenye gazeti la The Star, mzozo huo ambao upo mahakamani kwa miezi kadhaa, uamuzi utatolewa mwezi Juni iwapo maiti ya Kibaki itafukuliwa kwa ajili ya vipimo vya DNA.

Mwanamume kwa jina Jacob Ochola alielekea mahakamani akidai kuwa mtoto wa Kibaki na kutaka mgao katika mirathi ya kiongozi huyo aliyefariki Aprili 2022.

“Ochola pamoja na mwanamke mwenye hurefu za jina JNL walielekea kortini wakidai mgao katika utajiri wa Kibaki kwa hoja kwamba ni wazawa na Rais wa zamani. Tangu wakati huo wameiomba mahakama kuagiza uchunguzi wa DNA ili kuonyesha kuwa wao ni watoto wa aliyekuwa mkuu wa nchi,” ripoti hiyo ilisema.

Wanataka kutambuliwa kama watoto wake na wanufaika wa mali yake.

Ocholla na JNL wanataka mahakama iamuru uchunguzi wa DNA wa ndugu au baba.

Katika maombi ya kwanza, wanataka mahakama iwaelekeze pamoja na watoto wanne wa Kibaki kufanyiwa uchunguzi wa DNA ili kubaini kama wao ni watoto wa marehemu Rais.

Watoto hao ni Judy, James Mark Kibaki, David Kagai Kibaki na Anthony Andrew Githinji Kibaki.

Katika maombi ya pili na mbadala, wanataka mahakama iamuru kufukuliwa kwa mwili wa Kibaki kwa ajili ya ukusanyaji wa sampuli zitakazotumika katika uchunguzi wa DNA baba.

Mnamo Oktoba mwaka jana, pande zote zilimwomba Jaji Eric Ogola kuwapa muda wa kutatua suala hilo nje ya mahakama.

Mazungumzo hayo yalionekana kuwa hayajafanikiwa kufikia Desemba huku pande zote zikiiomba mahakama muda zaidi kutafuta suluhu nje ya mahakama.

Ogola aliagiza waripoti kortini kuhusu hatua zozote zilizochukuliwa kufikia Februari 29.

Watoto hao tangu wakati huo wamepinga majaribio ya kuufukua mwili wa Kibaki, wakisema kuufanyia uchunguzi wa DNA kutakiuka usiri wao.