Chuo Kikuu cha Kenyatta chavunja kimya kufuatia ajali mbaya iliyowaua wanafunzi 11

Naibu chansela alithibitisha kuwa wanafunzi kadhaa walipoteza maisha katika ajali hiyo.

Muhtasari

•KU ilitangaza kuwa tayari wametuma timu ya wataalam kushughulikia hali hiyo, kutoa taarifa sahihi na kuwasaidia manusura.

•Taasisi hiyo hata hivyo ilisema kuwa hawako katika nafasi ya kutaja idadi halisi au majina ya wahanga wa ajali hiyo.

Basi lililohusika katika ajali.
Image: HISANI

Chuo kikuu cha Kenyatta kimetoa taarifa, saa kadhaa baada ya basi lake kuhusika katika ajali mbaya kwenye barabara kuu ya Nairobi-Mombasa.

Katika taarifa iliyotolewa Jumanne asubuhi, uongozi wa taasisi hiyo ulithibitisha kutokea kwa ajali hiyo usiku wa Jumatatu na kutangaza kuwa tayari wametuma timu ya wataalam kushughulikia hali hiyo, kutoa taarifa sahihi na kuwasaidia manusura.

Naibu chansela, Profesa Paul K. Wainaina pia alithibitisha kuwa wanafunzi kadhaa walipoteza maisha katika ajali hiyo.

"Kwa kusikitisha, ripoti hadi sasa zinaonyesha kuwa kuna vifo vya wanafunzi. Chuo kikuu kilituma timu kutoka Kampasi Kuu na Kampasi ya Mombasa hadi eneo la ajali jana usiku ili kutathmini hali, kuwasaidia walionusurika na kutoa ripoti sahihi,” alisema Bw Wainaina kwenye taarifa.

Taarifa hiyo ilisema zaidi, "Timu hiyo inajumuisha madaktari wawili, maafisa wa matibabu, maafisa wa usalama wa chuo kikuu pamoja na wanafunzi na maafisa wa ustawi wa wafanyikazi. Baadhi ya wanafunzi waliojeruhiwa wako katika mchakato wa kutathminiwa uwezekano wa kuhamishwa hadi Nairobi kulingana na hali zao.

Taasisi hiyo hata hivyo ilisema kuwa hawako katika nafasi ya kutaja idadi halisi au majina ya wahanga wa ajali hiyo, lakini ilithibitisha kuwa baadhi ya wanafunzi walipoteza maisha.

Naibu chansela pia alichukua fursa hiyo kuzifariji familia zilizopoteza wapendwa wao na kusisitiza kuwa taasisi hiyo iko pamoja nao.

"Wakati huo huo, Chuo Kikuu kimeunda Dawati la Usaidizi katika Kituo cha Huduma ya Wanafunzi wa Biashara (BSSC) Chumba 151 na nambari ya rununu 020 2310709 au 0723352483 ili kujibu maswali tunapotoa msaada na usaidizi katika wakati huu mgumu," taarifa hiyo ilisema.

Takriban wanafunzi 11 wa Chuo Kikuu cha Kenyatta walifariki Jumatatu jioni katika ajali mbaya ya barabarani iliyohusisha basi lao la shule na trela, Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Voi Ibrahim Daffala alithibitisha.

Daffala alisema wanafunzi 10 walifariki papo hapo huku mwingine akikata roho hospitalini.

Wanafunzi 42 walipata majeraha mabaya huku wanne wakiwa na majeraha madogo.

"Ajali hiyo ilitokea wakati mvua kubwa ilikuwa ikinyesha. Lori lilijaribu kuondoka kutoka barabarani ili kuepuka mgongano wa uso kwa uso na kusababisha ajali," Daffala alisema.

Picha zilizofikia Radio Jambo zinaonyesha basi la shule liligongwa upande wa kushoto.