Mama aliyepoteza wanawe 3 kwenye ajali ya mashua ziwa Baringo aomba msaada kuwazika

“Watoto wangu walikuwa wananiambia mama sisi tukisoma tutakupeleka kiwango kingine hutakuwa tena na taabu.” mama ya watoto hao alisema kwa majonzi.

Muhtasari

• Mama huyo wa watoto wanne alisimulia matukio siku ya Jumapili kabla ya kuagana na watoto wake wanne ambao alipaswa kuandamana na misheni ya vijana katika Kisiwa cha Kokwa.

Mama aliyepoteza watu 4 kwenye ajali ya mashua
Mama aliyepoteza watu 4 kwenye ajali ya mashua
Image: Hisani

Familia moja katika kijiji cha Ilchamus kaunti ya Baringo iliyopoteza watu 4 kati ya 7 waliozama ziwa Baringo Jumapili iliyopita sasa inaomba msaada kwa ajili ya kuwazika wapendwa wao.

Jane Lekikenyi, mama aliyepoteza wanawe 3 pamoja na kakake mmoja alisema wanawe walikuwa wanaenda kanisani kabla ya msala huo kutokea na kugharimu maisha yao.

Lekikenyi anasema alipoteza mabinti zake Ruth, Martha na Abigael pamoja na kaka yake kwa jina Dennis aambao wote waliangamia katika ajali ya boti ziwani Baringo.

“Watoto wangu walikuwa wananiambia mama sisi tukisoma tutakupeleka kiwango kingine hutakuwa tena na taabu. Kwa sababu mimi nilikuwa nawategemea hawa watoto, sina mtu wa kumtegemea, lakiji vile walienda naomba tu Mungu anisaidie na atajua pahali ambapo ataniweka,” mama ya watoto hao alisema kwa majonzi.

Lekikenyi, mchungaji wa Kanisa la Revival Church Salabani, pia alipaswa kuwa kwenye mashua hiyo yenye ilizama pamoja na watoto wake lakini alibadili mawazo dakika za mwisho baada ya kupokea simu kutoka kwa askofu akimtaka ahudhurie mkutano.

Mama huyo wa watoto wanne alisimulia matukio siku ya Jumapili kabla ya kuagana na watoto wake wanne ambao alipaswa kuandamana na misheni ya vijana katika Kisiwa cha Kokwa.