Serikali kulipia gharama za hospitali za waathiriwa wa mkasa wa bawa la Mai Mahiu

Isaac Mwaura alithibitisha kwamba watu 45 walipoteza maisha yao na 73 walijeuriwa na wanapokea matibabu.

Muhtasari

• Mwaura alisema Kaunti ya Nairobi ndio iliyoathirika zaidi na mafuriko hayo.

• Jumla ya watu 147,000 waliachwa bila makao, ambayo ni 77% ya watu wote waliopoteza makazi nchini.

• Mafuriko ya ghafla yalitokea baaada ya maji kuvunja ukuta Jumatatu asubuhi.

Msemaji wa serikali Isaac Mwaura
Image: Hisani

Serikali italipa bili za hospitali za waathirika wa mkasa wa bwawa lilovunja kingo zake eneo la Mai Mahiu, msemaji wa serikali Isaac Mwaura amesema.

 Mwaura alikuwa akizungumza na waandishi wa habari huko Mombasa ambapo alithibitisha kwamba watu 45 walipoteza maisha yao na 73 walijeuriwa na wanapokea matibabu.

 "Bili zao zote za hospitali zitalipwa na serikali kwa roho ya mshikamano," alisema.

Mwaura alisema kuwa Kaunti ya Nairobi ndio iliyoathirika zaidi na mafuriko hayo huku watu 147,000 wakiachwa bila makao, ambayo ni 77% ya watu wote waliopoteza makazi nchini na serikali imeweka kambi 52 za watu waliopoteza makazi ili kuhudumia watu walioathirika.

Takriban watu 70 hawajulikani waliko kutokana na mkasa wa bwawa eneo la Mai Mahiu  kufikisha 91 idadi ya watu wasiojulikana waliko kote nchini. 

Mafuriko yaliokuwa  na  kasi ya juu yalisomba vitu na binadamu baada ya bwawa moja eneo la Mai Mahiu kuvunja kingo zake majira ya asubuhi. 

 

Msemaji wa serikali aliwahimiza wakenya kuwasaidia wenzao ambao wameathiriwa na mafuriko kote nchini na kuchukuwa tahadhari wakati huu wa mvua kubwa.