Wafanyikazi 79 wa kaunti ya Nyamira wapatikana na vyeti ghushi

Gavana Nyaribo alisema kwamba kati ya wafanyikazi 4,100 wa kaunti hiyo, wafanyikazi 245 walipandishwa vyeo bila mpangilio huku 79 wakipata kazi kwa kutumia vyeti bandia, idara ya afya ikiongozwa kwa vyeti ghushi vya kitaaluma.

Muhtasari

• Kaunti pia ilikuwa imeanza hatua za kinidhamu dhidi ya wafanyikazi waliopandishwa vyeo kinyume na utaratibu.

• Nyaribo alielezea mshtuko kwamba Idara ya Afya iliongoza kwa idadi ya wafanyikazi walio na vyeti ghushi vya kitaaluma, ambapo kesi 24 ziliripotiwa.

Gavana AMOS NYARIBO.
Nyamira// Gavana AMOS NYARIBO.
Image: Facebook

Serikali ya Kaunti ya Nyamira imewachukulia hatua za kinidhamu wafanyikazi 324 waliopatikana na vyeti ghushi vya masomo au wamepandishwa vyeo kinyume cha sheria, jarida la People Daily limeripoti.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, gavana Amos Nyaribo alisema tayari wafanyikazi 79 wamesimamishwa kazi baada ya kaunti kupoteza takribani shilingi milioni 4.5 kila mwaka kupitia upandishaji vyeo usiofuata utaratibu na vyeti ghushi.

Nyaribo alinukuliwa na toleo hiyo akisema kwamba kati ya wafanyikazi 4,100 wa kaunti hiyo, wafanyikazi 245 walipandishwa vyeo bila mpangilio huku 79 wakipata kazi kwa kutumia vyeti bandia.

Alisema serikali iliwasilisha kundi la kwanza la vyeti 2,800 vya Cheti cha Elimu ya Sekondari ya Kenya kwa Baraza la Kitaifa la Mitihani la Kenya ili kuhakikiwa na 79 vilipatikana kuwa ghushi.

“Vyeti 2,800 vya elimu ya baada ya sekondari pia vilikuwa chini ya uangalizi wa vyuo mbalimbali kote nchini. Hadi sasa kesi tatu za kughushi diploma na vyeti vya shahada zimeripotiwa”, alisema.

“Miongoni mwa tofauti ambazo zilibainishwa na KNEC ni pamoja na kubadilishwa kwa alama za wastani, kubadilishwa kwa alama za masomo na kutofautiana kwa misimbo ya vituo vya mitihani.

Katika baadhi ya matukio, nambari za fahirisi katika vyeti hazikuwa za maafisa huku wengine wakibadilisha majina kwenye vyeti na vyao,” Nyaribo aliambia wanahabari.

Nyaribo alielezea mshtuko kwamba Idara ya Afya iliongoza kwa idadi ya wafanyikazi walio na vyeti ghushi vya kitaaluma, ambapo kesi 24 ziliripotiwa.

Idara za Fedha na Menejimenti ya Utumishi wa Umma zilikuwa na idadi kubwa ya pili ya wafanyikazi walio na karatasi zenye mashaka huku kila moja ikirekodi kesi 13.

Nyaribo alithibitisha kuwa kaunti ilikuwa imewaarifu wafanyikazi walioathiriwa na sasa inaelekea kusimamisha mishahara yao.

Kaunti pia ilikuwa imeanza hatua za kinidhamu dhidi ya wafanyikazi waliopandishwa vyeo kinyume na utaratibu.