Shule 2,000 kukosa kufunguliwa tena leo - serikali

Hii inafuatia tathmini iliyofanywa na mamlaka husika kuhusu maandalizi ya shule, kufuatia mvua kubwa iliyonyesha.

Muhtasari

•Naibu msemaji wa Serikali Mwanaisha Chidzuga alisema licha ya hayo, serikali imeweka mikakati ya kuhakikisha wanafunzi kutoka shule zilizoathirika wanaendelea kupata elimu.

•Chidzuga alibainisha kuwa sehemu nyingi za nchi hazijaathirika pakubwa na kwamba masomo yanaweza kuendelea.

ya watoto wakielekea shuleni.
Picha ya maktaba ya watoto wakielekea shuleni.
Image: MAKTABA

Naibu msemaji wa Serikali Mwanaisha Chidzuga sasa anasema kuwa angalau shule 2,000 hazitafunguliwa Jumatatu, Mei 13.

Akizungumza kwenye Radio moja nchini, Chidzuga alisema hii inafuatia tathmini iliyofanywa na mamlaka husika kuhusu maandalizi ya shule, kufuatia mvua kubwa iliyonyesha.

Aliendelea kusema kuwa pamoja na hayo, serikali imeweka mikakati kuhakikisha wanafunzi kutoka shule zilizoathirika wanaendelea kupata elimu.

Chidzuga aliongeza kuwa moja ya hatua zilizochukuliwa na serikali ni kuwahamisha wanafunzi walioathirika hadi shule jirani.

“Kabla hatujafungua shule kulikuwa na mikakati tuliyoiweka mfano kuna idara inayoangalia ubora wa majengo inaitwa Public Works tuliyapeleka kwenye baadhi ya shule kuangalia yapo salama kwa wanafunzi kwenda. wengine walitoa ripoti zao na hivi tunavyozungumza shule 2,000 haziwezi kufunguliwa leo," alisema.

"Lakini haimaanishi kwamba watoto hao hawatapata nafasi ya kusoma. Tumewahamisha baadhi ya wanafunzi katika shule zilizo karibu. Na kuna mahali tumeweka mahema na madawati ili kuwa na madarasa ya muda."

Naibu msemaji wa serikali alisisitiza kuwa serikali haiwezi kuendelea kuchelewesha kuanza kwa muhula wa pili, licha ya mafuriko kuathiri zaidi ya kaunti 30.

Chidzuga alibainisha kuwa sehemu nyingi za nchi hazijaathirika pakubwa na kwamba kujifunza kunaweza kuendelea.

Alisema serikali inafanya kila iwezalo katika uwezo wake kuhakikisha Wakenya wanalindwa na shule zianze tena.

Pia alitoa wito wa uvumilivu na uungwaji mkono kutoka kwa Wakenya wote