Dereva aliyemvamia afisa wa polisi Kasarani akamatwa

Ian Njoroge alikamatwa kwenye nyumba moja katika eneo la Jacaranda.

Muhtasari

• Mshukiwa anatarajiwa kujibu mashtaka kadhaa ikiwemo jaribio la mauaji kwa afisa wa polisi.

•Koplo Ogendo alijitoa upesi na haraka kwa minajili ya usalama wake ila dereva alimfuata huku akimzushIa vurumai 


Crime Scene
Image: HISANI

Dereva aliyenaswa kwenye video akimshambulia afisa wa polisi hatimaye amekamatwa.  Ian Njoroge alikamatwa kwenye nyumba moja katika eneo la Jacaranda.

Inasemekana kuwa, Njoroge alikuwa katika pilkapilka za kutafuta usaidizi baada ya kung’amua kuwa anatafutwa na maaafisa wa polisi.

Mkuu wa trafiki katika eneo la Nairobi ,Bwana Vitalis Otieno alidokeza kuwa mshukiwa anafaa kujibu mashtaka kadhaa ikiwemo jaribio la mauaji kwa afisa wa polisi.

Kulingana na taarifa kutoka kwa polisi, tukio hilo lililofanyika katika eneo la Kamiti Road kwenye makutano ya Mirema  lilimuacha afisa huyo na majeraha ya kuuguza na bado anaendelea kupokea matibabu hospitalini.

Afisa wa polisi Koplo Jacob Ogendo, alikuwa kazini kama kawaida akiwa shughuli za kushughulikia trafiki ambapo aligundua gari moja likikaidi sheria ya barabara huku likileta msongamano na zogo kwenye barabara hiyo.

Alipokuwa anakaribia gari hilo, Koplo Jacob Ogendo  aliliona gari hilo likipinda kweny barabara na kukwama. Akitekeleza wajibu mwafaka, aliingia kwenye gari hilo akaketi mbele ya kiti cha abiria na akamwelekeza dereva huyo kuelekea kwenye kituo cha polisi.

Gari lilipokaribia duka kubwa la Quickmart, dereva alilisimamasha ghafla na kisha kutoa upanga kutoka chini ya kiti.

Koplo Ogendo alijitoa upesi na haraka kwa minajili ya usalama wake ila dereva alimfuata huku akimshambulia polisi huyo kwa mangumi na mateke ghaya ya kumuacha na majeraha kadha wa kadha ya kuuguza.

Tukio hilo liliwawacha wakazi wa eneo hilo vinywa wazi kwani ilikuwa ni kinaya kwa mwanachi wa kawaida kumvamia afisa wa polisi. Alipokuwa anavamiwa, wanachi wenye hamaki na hasira walitokea mara moja tayari kumsaidia afisa huyo wa polisi.

Njoroge alifyatuka mbio kama risasi na kutoweka mara moja baada ya kung’amua kuwa umati wa watu ulikuwa umekasirika kwa kitendo alichofanya na angeendelea kubaki, yamkini chuma chake kingesalia motoni.

Aliingia mitini ila juhudi zake ziliambulia patupu mpaka aliponaswa na maafisa wa polisi kisha kuzuiliwa kituoni.