Miili zaidi yafukuliwa Shakahola katika awamu ya tano ya ufukuzi

Idadi ya walioaga kwenye msitu wa Shakahola imefikia 436 baada ya miili 7 kufukuliwa kwenye awamu ya tano ya ufukuzi.

Muhtasari

•Awamu ya tano ya ufukuzi wa miili kwenye msitu wa Shakahola inaendelea baada ya kung'oa nanga Jumatatu 3,Juni 2024

•Maafisa wa DCI walipata miili saba zaidi, na hivyo kufanya idadi ya waliofariki kufikia 436.

Image: BBC

Miili saba zaidi imetolewa katika msitu wa Shakahola kaunti ya Kilifi na hivyo kuongeza idadi ya walioaga hadi 436 huku awamu ya tano ya uchimbaji huo ikianza.

Maafisa wa DCI waligundua makaburi matatu katika sehemu moja ya msitu ambapo miili 429 iliyohusishwa na mafundisho hatari ya kidini ilifukuliwa katika awamu nne zilizopita. Wakati wahasiriwa wengi wa mauaji ya Shakahola walikufa kwa njaa, wengine walinyongwa

Katika siku ya kwanza ya awamu hii, maafisa wa DCI walipata miili saba zaidi, na hivyo kufanya idadi ya waliofariki kufikia 436. Miili hiyo, inayoaminika kuwa wafuasi wa itikadi mbaya ya kidini inayohusishwa na kasisi mwenye utata Paul Mackenzie wa Good News International, ilitolewa katika makaburi matatu.

Miili ya kwanza iligunduliwa Aprili 2023 katika msitu wa Shakahola karibu na pwani ya Kenya, na kusababisha kukamatwa kwa mchungaji Paul Mackenzie ambaye anadaiwa kuwaongoza wafuasi wake kujiua kwa njaa ili "kukutana na Yesu".

Mackenzie  amekana mashtaka 191 ya mauaji, kuua bila kukusudia na ugaidi.Pia ameshtakiwa kwa mateso na ukatili wa watoto.