Gavana Wavinya atafuta maoni ya umma kuhusu marufuku ya muguka Machakos

"Ninakuja kwenu wakazi wa Machakos kutekeleza zoezi la ushiriki wa umma kuhusu Muguka, kwa sababu siwezi kupiga marufuku peke yangu," alisema.

Muhtasari

•Wito wa Gavana Wavinya unatokana na dhamira ya nchi nzima kukomesha kabisa uuzaji  wa Muguka ambao umehusishwa na kusambaratika kwa jamii.

•Marufuku ya muguka ilitangazwa kwa mara ya kwanza na Gavana wa Mombasa Abdulswamad Nassir, akiangazia unywaji wa dawa hizo za vichocheo Pwani, wakiwemo watoto wanaokwenda shule.

GAVANA WA KAUNTI YA MACHAKOS WAVINYA NDETI
Image: KWA HISANI

Gavana wa Machakos Wavinya Ndeti amekaribisha umma kujadili hatua ya kupigwa marufuku kwa Muguka katika kaunti hiyo.

Akizungumza wakati wa ibada kanisani Machakos siku ya Jumapili, alibainisha kuwa muguka umethibitishwa kuwa tishio katika jamii kwani vijana wengi wameathirika pakubwa.

 "Ninakuja kwenu wakazi wa Machakos kutekeleza zoezi la ushiriki wa umma kuhusu Muguka, kwa sababu siwezi kupiga marufuku peke yangu. Ninahitaji kuwasiliana nanyi ili kukubaliana kuhusu njia ya kusonga mbele," alisema.

"Dawa hizi zimeathiri vijana wetu. Ikiwa kila kanisa linaweza kuongea na vijana tutaleta mabadiliko. Ndio maana nilikuja na wazo la Huduma ya Vijana ya Machakos ambapo tutawapa mafunzo na kuwarekebisha wale walioathirika."

Wito wa Gavana Wavinya unatokana na dhamira ya baadhi ya nchi kukomesha kabisa uuzaji na matumizi ya Muguka ambao umehusishwa na kusambaratika kwa jamii.

Marufuku ya muguka ilitangazwa kwa mara ya kwanza na Gavana wa Mombasa Abdulswamad Nassir, akiangazia unywaji wa dawa hizo za vichocheo Pwani, wakiwemo watoto wanaokwenda shule.

Gavana wa Kilifi Gideon Mung'aro alifuata mkondo huo na vivyo hivyo marufuku hiyo ilitangazwa Kwale.

Vile vile, kaunti tatu za kaskazini mashariki za Wajir, Garissa, na Mandera zimedokeza kuungana na kaunti za pwani katika kuweka marufuku hiyo.

Waziri wa Kilimo Mithika Linturi hata hivyo amedokeza kwamba marufuku ya muguka katika kaunti  ni batili, akibainisha kuwa dawa hiyo ni zao lililoratibiwa kulingana na sheria ya mazao ya 2013 na kanuni za miraa 2023.