Rais Ruto atoa risala za rambirambi kwa waliofariki wakati wa maandamano bungeni

"Nikisikiliza kwa makini watu wa Kenya ambao wamesema kwa sauti kubwa kwamba hawataki chochote kuhusiana na Mswada huu wa Fedha wa 2024, ninakubali na kwa hivyo sitatia saini Mswada wa Fedha wa 2024."

Muhtasari

• "Nimekubali na kwa sababu tumeondokana nayo, tunahitaji kufanya mazungumzo kama taifa," alisema.

Image: screengrab

Rais William Ruto amekubali shinikizo na kusema hatatia saini Mswada wa Fedha wa 2024.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ikulu ya Nairobi, Ruto alisema kwamba amezisikia sauti na vilio vya wananchi na kukiri kwamba mswada huo hautatiwa saini na kuwa sheria, uamuzi ambao alisema aliafikiana na wabunge wa mrengo wa serikali katika mkutano uliofanyia awali.

Rais alisema wananchi wamezungumza.

"Nikisikiliza kwa makini watu wa Kenya ambao wamesema kwa sauti kubwa kwamba hawataki chochote kuhusiana na Mswada huu wa Fedha wa 2024, ninakubali na kwa hivyo sitatia saini Mswada wa Fedha wa 2024 na baadaye utaondolewa," alisema.

Vyanzo vya habari vya Ikulu hapo awali vilituambia kwamba Mkuu wa nchi pia amekataa kuidhinisha Mswada huo.

Kando na kutupiliwac mbali kwa mswada tata wa fedha 2024, rais Ruto pia alisikitika kufuatia vifo vya raia waliokuwa wakiandamana na kuuawa kwa kupigwa risasi katika majengo ya bunge.

Ruto alithibitisha kwamba takribani raia 6 walipoteza maisha yao katika mtafaruku huo ulioshuhudiwa Jumanne, na kutajwa kama umwagikaji damu mbaya zaidi kuwahi kutokea katika bunge la Kenya

Kando na hayo, Rais William Ruto ametuma rambirambi kwa familia na marafiki wa Wakenya waliopoteza maisha wakati wa maandamano ya Jumanne.

"Kwa niaba yangu mwenyewe, na ya Wabunge na Wakenya wengine, ninatuma risala zangu za rambirambi kwa familia zilizopoteza wapendwa wao kwa njia hii mbaya," alisema.