Joho amtaka Gachagua kujiuzulu kwa kudhalilisha idara ya NIS

"Kwa hivyo ningetamani kumuona akiongoza kwa mfano kwa kuwa wa kwanza kuwajibika na kujiuzulu badala ya kuomba kujiuzulu kwa watu wengine," alisema.

Muhtasari

•Joho alimkashifu Gachagua kwa kuelekeza  lawama kwa NIS, akisema huu sio wakati wa kunyoosheana vidole vya lawama bali kuvutana katika mwelekeo mmoja.

•Gachagua alikuwa amebainisha mnamo Jumatano, Juni 26, 2024, kwamba NIS ilikuwa ikiongozwa na watu wasio na uwezo ambao walikuwa wakimjulisha vibaya Rais Ruto kuhusu hisia halisi za umma

Hassan Ali Joho
Image: Intagram

Aliyekuwa gavana wa Mombasa Hassan Joho amemwambia Naibu Rais Rigathi Gachagua ajiuzulu muda tuu baada ya kukashifu Idara ya Kitaifa ya Ujasusi (NIS) kuhusu maandamano ya Mswada wa Fedha wa 2024.

Kupitia ukurasa wake wa X, Joho alimkashifu Gachagua kwa kuelekeza  lawama kwa NIS, akisema huu sio wakati wa kunyoosheana vidole vya lawama bali kuvutana katika mwelekeo mmoja.

"Baada ya kusikiliza kwa makini hotuba ya Naibu Rais jioni hii, ninapata usumbufu kwamba kiongozi wa hadhi yake angetoa matamshi hayo ya kizembe wakati ambapo serikali inahitaji kuonekana ikivuta upande mmoja," Joho alisema.

Gachagua alikuwa amebainisha mnamo Jumatano, Juni 26, 2024, kwamba NIS ilikuwa ikiongozwa na watu wasio na uwezo ambao walikuwa wakimjulisha vibaya Rais Ruto kuhusu hisia halisi za umma.

Naibu rais alifichua kwamba ilikuwa imechukua hasara ya maisha na uharibifu mkubwa wa mali kwa rais kukubaliana na kutoridhika kwa umma na Mswada wa Fedha wa 2024, akisema NIS ndiyo ya kulaumiwa.

"Kama nchi, tunajipata katika eneo lisilojulikana sana na kwa hivyo ni wajibu kwa uongozi wa nchi kujaribu kurejesha imani kwa raia wake badala ya kugawanya lawama za kushindwa ambazo zinafaa kumilikiwa na wao kwa pamoja," Joho aliongeza.

Gachagua alitoa wito kwa Rais Ruto kuwarejesha nyumbani wakurugenzi watatu ambao walikuwa wamefutwa kazi kutoka NIS wakiwemo wasaidizi wengine 13 ambao alisema walikuwa wametumwa tena kwa majukumu madogo afisini.

Hata hivyo, Joho alishikilia kuwa Gachagua alikuwa akilenga uongozi wa NIS isivyo haki na kwamba hotuba yake mjini Mombasa iliambatana na maneno ya kikabila.

"Ili kuifanya kuwa mbaya zaidi hisia za Bw. Rigathi Gachagua za ukabila na hilo ndilo jambo la chini kabisa ambalo taifa hili linahitaji kwa wakati huu," Joho alisema.

 "Kwa hivyo ningetamani kumuona akiongoza kwa mfano kwa kuwa wa kwanza kuwajibika na kujiuzulu badala ya kuomba kujiuzulu kwa watu wengine," alisema.

Haya yalijiri baada ya Gaachagua kumtaka Mkurugenzi Mkuu wa NIS Noordin Haji kujiuzulu kwa kile alichokiita kupotosha urais na kupotea kwa maisha na uharibifu wa mali nchini.