Maswali yaibuka kuhusu uhalali wa hotuba ya rais na naibu wake

Wananchi zaidi ya 129,000 walijiunga kwenye mtandao wa kijamii ili kuchambua hotuba ya rais William Ruto

Muhtasari

•Wengi walighadhabishwa wakati rais alinena ni watu sita waliaga kwenye maandamano ya juzi ambayo idadi iikuwa zaidi ya ishirini

•“Sasa huyo anaona hatukusoma historia? Baada ya siku 21 mswada huu utakua sheria. Anaona tukiwa wajinga sana,” aliandika 58 Kiddoh.

" Walikuwa wanafanya ambacho serikali ilikuwa inataka,"alisema naibu rais.

RAIS WILLIAM RUTO
Image: PCS

Vijana kupitia mitandao yao wamejitokeza kidete na kupinga hotuba ya rais William Ruto ambayo wanasema ni mojawapo ya mbinu ya kuwahadaa na kuwafumba macho wananchi.

Hotuba ya rais ya kufutilia mbali Mswada wa Fedha 2024, inafuatia siku moja baada ya yeye kuhutubia nchi kuwa taifa lilikuwa limeshambuliwa na majangili waliojipanga kwenye maandamano hayo.

“Nawasihi kama mzazi wenu ,enyi wanetu wa Gen Z maandamano ya kesho muyasitishe kwani rais amefutilia mbali Mswada wa Fedha 2024,” alisema naibu wa rais Rigathi Gachagua kwenye hotuba yake.

“Tutasikiliza tu mkisema mnaresign! Meanwhile, kesho masaa ni ile ile,” alisema Bud Company kupitia mtandao wa kijamii wa Instagram.

“Sisi sio wajinga wacha michezo ya kulaumiana! Ruto lazima aende!” Aliandika Musa Jones.

Fauka na hayo, wananchi zaidi ya 129,000 walijiunga kwenye mtandao wa kijamii ili kuchambua hotuba ya rais William Ruto. Wengi walighadhabishwa wakati rais alinena ni watu sita waliaga kwenye maandamano ya juzi ambayo idadi iikuwa zaidi ya ishirini.

“Rambirambi gani na amesema ni watu sita wameaga!” aliandika Swale.

“Sasa huyo anaona hatukusoma historia? Baada ya siku 21 mswada huu utakua sheria. Anaona tukiwa wajinga sana,” aliandika 58 Kiddoh.

Kwenye hotuba ya naibu rais, mkurugenzi mkuu wa Huduma ya Kitaifa ya Ujasusi Noordin Hajji, alilaumiwa kwa kukosa kumpa rais ushauri unaofaa kuhusiana na mambo nyeti ya nchi.

"Nawaomba msiwaadhibu wabunge wetu, walifanya kilicho sahihi kwa mjibu wa sheria za chama. Walikuwa wanafanya ambacho serikali ilikuwa inataka,"alisema naibu rais.

Hali hii imezidi kuchipua mdahalo mkali hasa kwa wabunge kuwa iwapo wanafanya kile ambacho serikali inataka ama wanawakilisha wananchi waliowachagua?