Rais wa Uganda, Museveni naye akataa kutia saini mswada wa fedha wa mwaka 2024

Mswada huo wa matumizi ya serikali ulikuwa umepitishwa na bunge Mei 16 ila Jumatatu wiki hii, Museveni aliambia baraza lake la mawaziri kwamba hatotia saini kuwa sheria,

Muhtasari

• Mswada huo wa matumizi ya serikali ulikuwa umepitishwa na bunge Mei 16 ila Jumatatu wiki hii, Museveni aliambia baraza lake la mawaziri kwamba hatotia saini kuwa sheria,

Museveni
Museveni
Image: X

Wakati suala la mswada wa fedha wa mwaka 2024 likizidi kuzua joto kali la kisiasa humu nchini, katika taifa jirani la Uganda, rais Yoweri Museveni naye amearifiwa kudinda kutia saini mswada wa fedha wa mwaka huu.

Kwa mujibu wa jarida la The New Vision, Museveni aliweka wazi kwamba hatotia saini mswada huo kuwa sheria hadi pale uwazi utakapotolewa kuhusu pesa zilizotengwa upya na bunge, Zaidi ya bilioni 750 pesa za Uganda.

“Rais katika tamko la wazi alituambia kwamba hatotia saini mswada huo hadi pale suala kuhusu kutengwa upya kwa Sh 750b na kamati ya bunge kuhusu bajeti linaangaziwa na kutathminiwa upya,” chanzo kiliambia jarida hilo.

Waziri wa fedha, Matias Kasaija alithibitisha kwa The New Vision kwamba ni kweli rais Museveni amedinda kutia saini mswada kuwa sheria akisema kwamba hana ruhusa Zaidi ya kuzungumzia kilichozungumziwa kwenye baraza la mawaziri kwenye vyombo vya habari.

“Ninalifahamu hilo kwa sababu rais alituambia katika baraza la mawaziri kwamba anaurudisha mswada huo, ila kwa sasa siwezi kuzungumzia Zaidi hadi pale nitakapopata idhini yake,” Kasaija alinukuliwa.

Mswada huo wa matumizi ya serikali ulikuwa umepitishwa na bunge Mei 16 ila Jumatatu wiki hii, Museveni aliambia baraza lake la mawaziri kwamba hatotia saini kuwa sheria, akisema wabunge walihitilafiana na bajeti hiyo bila idhini kutoka kwa uongozi wa rais.

Wakati hayo yakijiri, nchini Kenya hali ni tete siku moja baada ya rais Ruto kutangaza uamuzi wa kuutupilia mbali mswada huo, kwa kile alisema amekwishasikiliza sauti za wananchi.

Licha ya kutangaza hivyo, baadhi ya Wakenya leo hii bado wamejitokeza katika maeneo mbalimbali nchini wakiandamana kwa kile wanahisi tamko la rais huenda likabadilika kulingana na vifungu vya katiba.