Wakazi wa Rongai warai serikali ikarabati barabara zao

Wamesema kuwa barabara zao zinazidi kuchakaa kila kukicha.

Muhtasari

•"Ahadi ni deni na dawa ya deni ni kulipa. Hizi barabara zetu 2022 zilikuwa kwenye hali hii hii tunayoshuhudia leo." Alisema mkazi mmoja.

•Msongamano wa magari unazidi kupamba moto huku wakazi wakilalama hali mbaya inayoshuhudiwa hasa mvua kubwa inaponyesha.

Hali mbovu ya barabara Ongata Rongai
Image: JOSEPH OMBATI

Baadhi ya wakazi wa Ongata Rongai, Kajiado wamelalamika kuhusu hali mbaya ya barabara zao ambazo wanadai zimezidi kuharibika kila kukicha.

Mashimo yameonekana yakizidi kuchipuka hivyo basi kutatiza uchukuzi wa bidhaa pamoja na  abiria kutoka eneo moja hadi lingine.

“Serikali hii, ikiingia, ilikuwa na na ahadi nyingi na kwa kawaida,ahadi ni deni na dawa ya deni ni kulipa. Hizi barabara zetu 2022 zilikuwa kwenye hali hii hii tunayoshuhudia leo.

Kwani ushuru tunatoa kuenda kulisha tumbo za mabwanyeye wala sio kutumikia wananchi kulingana na jinsi walivyoahidi,” alisema mkazi mmoja.

Fauka ya hayo, hali mbovu ya barabara imezidi kuleta mtafaruku kwani msongamano wa magari unazidi kupamba motohuku wakazi wakilalamika kuhusu hali mbaya inayoshuhudiwa hasa mvua kubwa inaponyesha.

“Barabara yetu ya Gataka inakuwa mbaya mvua kubwa inaponyesha. Unapata kuna matope, hivyo basi kufanya usafiri wa miguu kuwa muhali.

Ukipanda pikipiki unaweza anguka juu ya maji taka yanatapakaa na kukithiri sehemu kubwa ya nchi.” Alisema manamba mmoja.

“Shida kubwa tena, huwa ni wakati unauza vyakula vya mitaani kisha vumbi inaingia kwa vyakula wanavyotia tumboni wananchi.

Tunaomba serikali iingilie kati iunde barabra zetu ili mazingira na mandhari yawe safi.

Iwapo mazingira yatakuwa chafu kunaweza kuzuka maradhi kama vile kipindupindu.” Alisema mamamboga.

Huku malalamishi haya  yakiibuliwa, taifa la Kenya limezidi kushuhudia mwamko mpya wa vijana wa kizazi cha Gen Z wanasimama kidete kupinga uongozi mbaya na ubadhirifu wa mali ya wananchi.