Ruto atangaza siku 3 za maombolezo ya kitaifa kufuatia vifo vya wanafunzi 17

Hii ni kufuatia vifo vya wanafunzi 17 katika shule ya Hillside Endarasha Academy iliyo kaunti ya Nyeri, Alhamisi usiku.

Muhtasari

•Rais aliagiza bendera za Kenya na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zipeperushwe nusu mlingoti wakati wa maombolezo hayo.

•Rais Ruto alisema kuwa kufiwa kwa watoto wa umri mdogo kwa namna hiyo ni msiba usio na kifani.

Rais William Ruto
Rais William Ruto
Image: PCS

Rais William Ruto ametangaza kipindi cha siku tatu cha maombolezo ya kitaifa.

Hii ni kufuatia vifo vya wanafunzi 17 katika shule ya Hillside Endarasha Academy kaunti ya Nyeri, siku ya Alhamisi usiku.

Wanafunzi hao walifariki baada ya moto kuzuka katika bweni moja la shule hiyo mwendo wa saa tano usiku.

"Kama adhimisho nzito la alama isiyofutika iliyoachwa katika ufahamu wa taifa na roho za watoto kumi na saba walioaga, Kenya itaadhimisha siku tatu za maombolezo ya kitaifa," Ruto alisema kwenye taarifa.

Rais aliagiza bendera za Kenya na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zipeperushwe nusu mlingoti wakati wa maombolezo hayo.

Bendera zitapeperushwa nusu mlingoti kuanzia alfajiri ya Jumatatu, Septemba 9, 2024 hadi machweo ya Jumatano, Septemba 11, 2024.

Hili litafanywa katika Ikulu, sehemu zote za kidiplomasia za Kenya, majengo ya umma, viwanja vya umma, vituo vyote vya kijeshi, vituo vya polisi, vyombo vyote vya wanamaji vya Jamhuri ya Kenya na katika eneo lote la Jamhuri ya Kenya.

Rais Ruto alisema kuwa kufiwa kwa watoto wa umri mdogo kwa namna hiyo ni msiba usio na kifani.

Pia alichukua fursa kutoa rambirambi kwa familia zilizopoteza watoto wao kwenye moto huo.

"Wanapoomboleza na kuhuzunika, tunawakabidhi kwa upendo na neema ya Mwenyezi, kwani Yeye pekee ndiye anayeweza kuwapa nguvu na uponyaji wanaohitaji katika saa hii ya giza zaidi ya maisha yao," rais alisema.

Rais alieleza huruma zake kwa wanafunzi walionusurika katika tukio hilo na wavulana 14 waliopata majeraha.

Kwa mujibu wa Rais, watoto walioangamia walikuwa kati ya umri wa miaka tisa na 13, wa darasa la 4 hadi 8.

Ruto alisema hasara hiyo inaibua hisia za kipekee za hasira, uchungu, huzuni na utupu.

Alisema tukio hilo linailazimu serikali kuhakikisha uwajibikaji katika shule zote nchini na kuchukua kila hatua ili kulinda maisha ya watoto wanaokwenda shule.

Pia alizihakikishia familia zilizoathiriwa kuwa kila rasilimali ya matibabu ya umma itakuwa mikononi mwao ili kuhakikisha kuwa watoto wote waliojeruhiwa wanapata huduma ya hali ya juu.

"Kama Rais wako, naahidi kwamba maswali magumu ambayo yamekuwa yakiulizwa kama vile mkasa huu ulivyotokea na kwa nini majibu hayakufika kwa wakati yatajibiwa; kikamilifu, ukweli na bila woga wala upendeleo," alisema.

Aidha, kiongozi wa nchi aliihakikishia taifa kuwa watu na vyombo vyote vilivyohusika vitawajibishwa, na akaongeza kuwa serikali itafanya kila linalohitajika ili kuhakikisha nchi haitajipata tena katika janga la aina hiyo.

"Hizo ni hatua ambazo lazima na zitachukuliwa katika siku zijazo. Kwa sasa, taifa letu lazima liomboleze na kuwaheshimu vijana wetu 17 waliopoteza maisha, na lazima tusimame kwa mshikamano na familia zao, marafiki, jamaa na wanafunzi wenzao," alisema.

Siku ya Ijumaa asubuhi, Wakenya waliamkia habari za kusikitisha za mkasa wa moto ambao ulikuwa umegharimu maisha ya takriban wanafunzi 17 katika shule ya msingi ya kibinafsi katika Kaunti ya Nyeri.

Ijumaa asubuhi,Rais Ruto na naibu wake Rigathi Gachagua tayari walikuwa wametuma risala zao za rambirambi kwa familia hizo na kuomba uchunguzi ufanyike kuhusu tukio hilo.