Siasa za Mlima: Njuri Ncheke wambwaga Gachagua na kumtawaza Kindiki kama msemaji

Wazee hao zaidi ya 2,000 walitangaza kujiondoa kwa Gachagua na kuweka wazi kwamba watakuwa wanamuunga mkono CS Kindiki kama msemaji wa maslahi ya eneo pana la Mlima Kenya.

Muhtasari

• Hata hivyo, awali kulishuhudiwa mgawanyiko kati ya wawakilishi wadi walioandaa mkutano katika kaunti ya Murang’a baadhi wakiunga mkono Kindiki na wengine wakiganda na Gachagua.

GACHAGUA NA KINDIKI.
GACHAGUA NA KINDIKI.
Image: FACEBOOK//GACHAGUA

Siasa za ukanda wa Mlima Kenya zinazidi kuchukua mikondo tofauti kila kukicha baada ya makundi mawili kuibuka kila moja likitangaza kuwa msemaji wao.

Kundi moja limeibuka na kudai kumtawaza waziri wa usalama wa ndani profesa Kithure Kindiki kama msemaji wa eneo la Mlima Kenya huku kundi jingine likikwama na naibu rais Rigathi Gachagua kama msemaji wao.

Hatua ya hivi punde ni ile ya wazee wa jamii ya Ameru, Njuri Ncheke, wapatano zaidi ya 2,000 kuandaa mkutano Jumatano na kutangaza kujikata kutoka kwa mrengo wa Gachagua na kujibwaga nyuma ya Kindiki.

“Tuko na kijana wetu, mtoto wetu tuliyemzaa kutoka Meru, ambaye ni Kithure Kindiki. Siku ya leo Njuri Ncheke katika idadi yao tumemtangaza kama kiongozi wetu, kama msemaji wetu kwamba yeye ndiye atakuwa nyota yetu, ndiye atakuwa muunganishi wa eneo lote la Mlima Kenya na serikali kuu,” wzee hao walisema kwa sauti moja.

Hata hivyo, awali kulishuhudiwa mgawanyiko kati ya wawakilishi wadi walioandaa mkutano katika kaunti ya Murang’a baadhi wakiunga mkono Kindiki na wengine wakiganda na Gachagua.

“Mradi wa maslahi ya MCAs umekwama na tumejairbu kila mtu imeshindikana. Na sasa tunasema kama inamaanisha kupitia kwa Kindiki ndio tutaangaziwa basi ni sawa. Mkutano wetu ulikuwa kuhusu jinsi ya kuungana na CS Kindiki kuleta maendeoe katika eneo hili letu,’ mrengo wa MCAs wanaosimama na Kindiki walisema.

Hata hivyo, wenzao wanaomuunga Gachagua mkono walipinga kwamba ajenda kuu za mkutano huo haikuwa hiyo.

“Tumefika sisi wote na kujaa hapa, lakini ile ajenda ambayo tuliitiwa jana sio ile ambayo tumeikuta mezani leo. Na hii vile tumeona ni njama ya kujaribu kumpiga chini naibu wa rais Rigathi Gachagua. Sisi kama MCAs na viongozi wa mashinani, hiyo hatutakubali,” mrengo wa Gachagua ulisimama tisti.