Mwanaume ang'olewa macho katika mzozo wa mapenzi Kisii

Kengere alisema alishambuliwa na watu waliompata nyumbani kwa mchumba wake.

Muhtasari

•Polisi walisema Kengere alipatikana akirandaranda kwa nia mwendo wa saa nane usiku wa kuamkia Jumanne na kwamba alikimbizwa hospitalini huku akivuja damu machoni.

•"Nilikuwa ndani ya nyumba wakati mwanamume fulani alivamia na kunishambulia," Kengere alisema.

Simon Kengere akipata nafuu katika kitanda chake hospitalini Ogembo, Kisii baada ya kushambuliwa. Alisema kundi la watu lilimvamia machoni baada ya kupatikana katika nyumba ya mpenzi wake
Simon Kengere akipata nafuu katika kitanda chake hospitalini Ogembo, Kisii baada ya kushambuliwa. Alisema kundi la watu lilimvamia machoni baada ya kupatikana katika nyumba ya mpenzi wake
Image: MAGATI OBEBO

Mwanamume mmoja mwenye umri wa makamo kutoka eneo la Magena, kaunti ya Kisii anapigania macho yake baada ya umati wa watu kumvamia katika shambulizi linaloshukiwa kuwa mzozo wa kimapenzi.

Polisi, hata hivyo, walisema Simon Kengere 40, alipatikana akirandaranda kwa nia mwendo wa saa nane usiku wa kuamkia Jumanne na kwamba alikimbizwa hospitalini huku akivuja damu machoni.

“Iliripotiwa alivamiwa na kundi la watu baada ya kupatikana akivunja nyumba. Maafisa wetu walijibu mara moja, wakamuokoa na kumkimbiza hospitalini ambako anahudumiwa,” alisema Charles Opondo, Kamanda wa Polisi Kaunti Ndogo ya Kenyenya.

Hata hivyo, alifafanua kuwa kulikuwa na tetesi nyingi kuhusu tukio hilo na kuongeza kuwa wanaendelea kufanya uchunguzi.

“Kuna wengine wanasema alikutwa kwenye nyumba ya mwanamke fulani huku wengine wakisema ni mwizi na wengine bado wanasema ni mchawi, tunaendelea na uchunguzi na ingekuwa mapema sana kutoa sababu kamili ya kwanini alishambuliwa,” alisema Opondo.

Alisema hata hivyo bado wanaangalia taarifa hizo zote huku wakitafuta kutofautisha ukweli na propaganda.

"Tutaangalia hilo pia, wakati huo huo tunaendelea na uchunguzi," alisema kupitia njia ya simu Jumanne.

Opondo alisema Kengere alikimbizwa katika Hospitali ya Gucha, eneo la Ogembo kwa matibabu ya dharura lakini kufikia Jumanne jioni familia ilikuwa inatafuta rufaa ili apelekwe katika kituo tofauti cha afya kwa matibabu ya hali ya juu, Opondo aliongeza.

Akiwa Gucha, Kengere alisema alitobolewa macho na watu waliompata kwenye nyumba ya mchumba wake.

"Nilikuwa ndani ya nyumba wakati mwanamume fulani alivamia na kunishambulia," aliwaambia waandishi wa habari kutoka kwa kitanda chake hospitalini.

Alikuwa na madoadoa ya damu machoni.

Opondo alisema shambulio la mwanamume huyo halifanani na shambulio la Alhamisi usiku la mtoto Junior Sagini ambaye aling'olewa macho katika shambulio la kikatili.

Washukiwa wawili tayari wamewekwa chini ya ulinzi kwa jaribio la mauaji katika tukio la Sagini.