Hatutakusahau! - DP Gachagua amuahidi waziri wa elimu anayeondoka, prof Magoha

Gachagua alimwambia Magoha kwamba watazidi kumtafuta kutolea ushauri kuhusu CBC hata baada ya kuachia ngazi kama waziri wa elimu.

Muhtasari

• Ninakubaliana huenda tuko sawa katika mambo mengi, katika kuzungumza mawazo yetu wazi wazi - DP Gachagua alisema.

DP Gachagua amhakikishia Magoha kuwa serikali ya Kenya Kwanza haitomsahau
DP Gachagua amhakikishia Magoha kuwa serikali ya Kenya Kwanza haitomsahau
Image: Tweeter

Naibu rais Rigathi Gachagua amemhakikishia waziri wa elimu anayeondoka profesa George Magoha kwamba serikali ya Jubilee haitamsahau na wala haina haraka ya kumvua mamlaka hayo.

Akizungumza wakati wa kikao cha uzinduzi wa kikosi kazi cha wanachama 42 cha kupitia Mtaala mpya wa CBC, DP Gachagua alisema kwamba kama serikali mpya, hawana haraka ya kumtupilia nje Magoha kwani yeye amekuwa nguzo muhimu katika kuhakikisha ufaafu na kufaulu kwa mtaala huo mpya ambao kwa mara nyingi umeibua utata katika utekelezwaji wake.

“Mimi ningependa kumshukuru waziri anayeondoka kwa kujitolea kuweka timu hii pamoja. Umeonesha uzalendo kwamba licha ya kuwa mbioni kuachia ofisi hii, hukusema kwamba acha wengine waje waendelee bali umesimama imara kuhakikisha kwamba mchakato wote unaendelea kwa njia nzuri. Na ningependa kukuhakikishia kwamba hatuna haraka ya kukuvua mamlaka, chukua muda wako sababu hii ni nchi yako na hii ni serikali yako,” DP Gachagua alimwambia.

Naibu huyo wa rais ambaye amejijengea jina kutokana na kuwa na misimamo mikali pasi na kutishiwa au kuzuiliwa kuongea fikira na mawazo yake alisema kwamba yeye na waziri Magoha wanawiana katika kipengele hicho.

Alisema kuwa katu hawawezi kumsahau Magoha kwa mchango wake na hata kama kuna waziri mpya anayekuja kuchukua mikoba hiyo, bado watazidi kumtafuta kwa ushauri wakati atakapohitajika.

“Ninakubaliana huenda tuko sawa katika mambo mengi, katika kuzungumza mawazo yetu wazi wazi, tofauti ni kwamba ile serikali uliyokuwa unafanyia kazi hungezungumza ukweli kabla ya kuzuiliwa, na hii serikali yetu mtu anasema ukweli jinsi ulivyo,” Gachagua alisema.