Hakutakuwa na muda wa mama mboga kwenye serikali ya Ruto - Ole Kina

Alisema kwamba ili mtu kuteuliwa na Ruto, ni sharti awe na mamilioni kiasi kutokana na mawaziri waliohojiwa na kuweka wazi thamani ya utajiri wao.

Muhtasari

• Seneta huyo wa Narok alisema kwamba Ruto alitumia dhana hiyo ya mama mboga na mtu wa boda boda kama ulaghai wa kisiasa katika kampeni.

Ole Kina asema Ruto aliwahadaa wananchi
Ole Kina asema Ruto aliwahadaa wananchi
Image: Facebook

Seneta wa Narok Ledama Ole Kina alionekana kugusia suala la uhakiki wa baraza la mawaziri katika serikali ya Ruto, zoefu ambalo linaendelea siku yake ya pili katika bunge la kitaifa.

Ole Kina alisema kwamba amestaajabishwa na thamani kubwa ya mawaziri wa Ruto kinyume na dhana ambayo aliwajengea wananchi kuwa serikali itakuwa ya mahasla.

 Akionekana kusuta baraza hilo la mawaziri ambao wengi wamenukuu thamani yao kuwa ya mamilioni ya oesa, Ole Kina alisema kwamba hakutakuwa na muda wa kina mama wauza mboga au hata wahudumu wa bodaboda kwenye serikali ya Ruto.

Alisema rais alitumia dhana ya watu wenye kipato cha chini na ambao ni wapambanaji kama ngazi ya kumkweza uongozini kwa kutumia kura za wapambanaji hao lakini hatoweza kuwakumbuka wala kuwathamini hata kidogo.

“Tunachojifunza kutoka siku ya kwanza ya uhakiki wa walioteuliwa kuwa CS ni kwamba unapaswa kuwa na thamani ya mamilioni mia chache kuzingatiwa. Hakutakuwa na muda wa Mama Mboga na Mtu wa Boda................. Ule ulikuwa ni ulaghai wa kampeni!” Ole Kina alisema.

Kisheria, baada ya rais kuteua mawaziri wake, mchakato wa kuwahoji na kuwakagua unaanza katika bunge la kitaifa, hii ikiwa ni chini ya mwezi mmoja tangu kuteuliwa rasmi na rais.

Mawaziri hao wateule ambao mpaka sasa wamepitia mchakato wa kuhojiwa na kamati ya bunge ni mkuu wa mawaziri Musalia Mudavadi, Kithure Kindiki wa usalama wa ndani, Aden Duale wa ulizni miongoni mwa wengine ambao wanatarajiwa kufika mbele ya wabunge hao wiki hii.

Swali kuu ambalo mawaziri hao wote wamepitishwa kwalo ni kutaka kueleza thamani ya utajiri wao ambao wengi wameonekana kutaja mamilioni ya utajiri.

Vile vile, hilo limeonekana kumkasirisha mbunge wa Embakasi East ambaye amewasuta pamoja na rais Ruto kwa kusema kwamba alikuwa anadanganya Wakenya kuwa serikali yao itakuwa ya watu wenye kipato cha chini ambao ni wapambanaji lakini mawaziri wake wote ni watu wenye thamani ya mamilioni.

Owino alisema kwamba yeye hawezi tambua hilo la kumalizia kuwa utajiri wake uko mbinguni.

“Hii Kenya kuna HUSTLERS na kuna SUFFERERS. Hustlers ni wezi wanaohojiwa kwa sasa huku wanaoteseka ni wakenya waliochini. Utajiri wangu uko mbinguni,” Babu Owino alisema.