Video ya mwanafunzi akichapwa viboko huku akilia kwa huruma yazua ghadhabu mitandaoni

Katika video hiyo, mwanafunzi anaonekana amefungwa kamba mikononi pamoja na miguuni huku akishambuliwa vikali na walimu na chifu.

Muhtasari

• Mwanaume mmoja anayedhaniwa kuwa chifu anaonekana akimcharaza vikali mwanafunzi huyo pasi na kujali kilio chake cha huruma.

Wanamitandao wamekasirishwa na video moja ambayo ilipakiwa kwenye ukurasa wa Twitter ikionesha mwanaume aliyedhaniwa kuwa chifu mmoja akishirikiana na walimu kumcharaza mtoto viboko.

Katika klipu hiyo, mwanafunzi huyo ambaye ni mtoto wa kiume alionekana amefungwa Kamba ambayo ilikuwa imeunganisha pamoja mikono na miguu, kumwaacha amejipinda kama upinde na hivyo kufanya kucharazwa  kwake upande wa makalio kuwa rahisi.

 Kitendo hicho kinadhaniwa kutokea katika shule moja eneo la Kisii, kutokana na kwamba mwanafunzi huyo anasikika akilia kwikwi huku akiomba radhi kwa lugha ya Kisii na kumtaja mwanaume huyo kama chifu huku akiomba radhi.

Walimu hao wanasikika wakisema kwamba viboko bado havijatembezwa katika makalio ya mtoto huyo huku wakizidi kusomba voboko zaidi na chifu huyo akizidisha kumtia adabu kwa njia ya kuudhi, ambapo walimu pia wanashirikiana naye na kumshambulia vikali.

Kutokana na kile ambacho wanakitaja kuwa makosa ya mtoto huyo, ni kama alichukua panga na kutaka kumshambulia mtu baada ya kukorofishana, kupelekea kukabidhiwa kiban hicho cha adhabu kwa njia ya kufungwa Kamba mikono na miguu kwa pamoja.

“Chifu nionee huruma siwezi kurudia tena,” kijana huyo anasikika akilia lakini aliokuwa anawalilia ndio mwanzo wanazidisha mashambulizi kwenye makalio yake kwa viboko.

Kitendo hicho kiliwagadhabisha watumizi wa Twitter ambao walipinga vikali na kusema kwamba hiyo si njia ya kumnyoosha mtoto kutoka njia ya makossa hadi kwenye njia salama.

“Makosa sana. Mzee huyu mtoto anaweza kupata haki? Hii sio nidhamu” mmoja kwa jina la Nyakiana alifoka.

“Vibaya sana na watu wanatakiwa kuacha upuuzi huu,” Mageto Dominic alisema.

Ikumbukwe hii si mara ya kwanza kwa video kama hizo kusambazwa zikiwaonesha watoto wakichapwa kwa njia kama hiyo, kwani miezi mitatu iliyopita video ilisambazwa mwanafunzi wa shule moja akililia haki baada ya kuchapwa na kuachiwa majeraha mabaya na walimu.

Nchini Kenya, kumchapa mtoto kwa njia kama hiyo ni kinyume na sheria baada ya kuharamishwa miaka michache iliyopita.