Kirinyaga: Mama aliyekwenda kufanya kazi Qatar aomboleza watoto wake 2 walioungua moto

Nahitaji maombi yenu kwa wingi, siwezi kustahimili hali hii - Wanjiku alilia.

Muhtasari

• Natamani mmoja wao angesalimika hata! Kwanini mimi Mungu kwanini?” Wanjiku aliomboleza.

Image: Screengrab, YouTube//Inooro TV

Hakuna uchungu kama mama kupoteza uzao wa tumbo lake, hata kwa maneno hauelezeki!

Mwanamke Mkenya anayefanya kazi nchini Qatar hana faraja baada ya watoto wake wawili wachanga kufariki katika nyumba iliyoteketea kwa moto wikendi iliyopita.

Mwanamke huyo kwa jina Pesh Wanjiku kutoka kaunti ya Kirinyaga alipakia video yenye picha za watoto hao wake wawili ambao waliteketea hadi kufa katika nyumba iliyoshika moto.

Watoto hao, msichana na mvulana wa kati ya miaka 3 hadi 5 walifariki katika mkasa huo ambao mama yao ambaye yuko ughaibuni kwa ajili ya kuwatafutia sasa ameshindwa kuzuia hisia zake huku akilia kwa majonzi kwamba hata mmoja angebaki.

“Nahitaji maombi yenu kwa wingi, siwezi kustahimili hali hii. Nilikuja kutafuta pesa kwa ajili ya watoto wangu, lakini nitakwenda kuwazika! Hii itawezekanaje? Natamani mmoja wao angesalimika hata! Kwanini mimi Mungu kwanini?” Wanjiku aliandika kwenye video hiyo ya kuliza.

Katika kisa hicho kilichotokea usiku wa Jumapili, nyanyake watoto hao ambao alizungumza na kituo kimoja cha runinga kwa lugha ya Kikuyu alisema kwamba watoto hao walikuwa wamemaliza kula na ndio walikuwa wanaelekea kulala kabla ya moto huo kuzuka.

“Watoto hao walikuwa na chakula cha jioni na baba yao, naye akawapeleka kitandani. Hakuwasha moto wala jiko, na baada ya kuwalaza, alienda kuongea na babake kuhusu kazi,” Nyanyakec watoto alisimulia, huku akidokeza kwamba huenda kuna mtu alivizia nyumba hiyo na kuitia moto kwa lengo la kuwaangamiza waliokuwemo ndani.