Sonko ajivunia kuhitimu chuo kikuu kwa binti aliyemuasili akiwa na miaka 5

Sonko alieleza kuwa alimchukua binti huyo baada ya kufiwa na wazazi wake akiwa na umri wa miaka 5 kutoka kaunti ya Kitui.

Muhtasari

• Ameishi nasi kama binti yetu wa kulea tangu wakati huo, tumempeleka shuleni na leo anahitimu - Sonko.

Sonko amsherehekea binti aliyemuasili kuhitimu chuo kikuu
Sonko amsherehekea binti aliyemuasili kuhitimu chuo kikuu
Image: Instagram

Aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko kwa mara nyingine ameonesha furaha yake baada ya binti aliyemuasili akiwa na umri wa miaka 5 kufanikiwa kuhitimu elimu ya chuo kikuu.

Akifichua habari hizi za kufurahisha kupitia kurasa za mitandao yake ya kijamii, Mike Sonko alisema kwamba binti huyo kwa jina Janet Kaingi alipata makazi mapya katika familia yake akiwa na umri wa miaka 5 baada ya kufiwa na wazazi wake katika kaunti ya Kitui miaka kadhaa iliyopita.

Sonko alimkumbatia na kumchukua kama mtoto wake na kuanza kumsomesha kutoka shule ya msingi hadi mwishoni mwa wiki jana kutoka chuo kikuu cha Daystar na shahada ya Kwanza ya uratibu wa mipango ya Biashara na Ununuzi.

“Ameishi nasi kama binti yetu wa kulea tangu wakati huo, tumempeleka shuleni na leo familia yangu inapenda kumsherehekea kwa ujumbe maalum anapohitimu,” Sonko alimwandikia binti huyo.

“Umekuwa sehemu ya familia yetu tangu umri mdogo. Tumekuona ukifanikisha mafanikio makubwa kutoka Shule ya Msingi ya Baraka Buruburu hadi Arya girls parklands na leo ukihitimu na Shahada ya Kwanza ya uratibu wa mipango ya Biashara na Ununuzi kutoka Chuo Kikuu cha Daystar. Hatutawahi kujivunia kama wazazi wako. Endelea kutufanya tujivunie hata unapoingia katika ulimwengu wa kweli, na kumbuka daima una familia ndani yetu. Hongera binti!” Sonko alimazilia.

Hii si mara ya kwanza kwa mhisani huyo kujitokeza bayana na kutoa msaada kwa makundi ya watu kutoka matabaka mbali mbali ya maisha.

Kupitia wakfu wake wa Sonko Rescue Team, mwanasiasa huyo amekuwa akitoa misaada ainati na kusifiwa kuwa mmoja wa watu wenye moyo wa kusaidia wakati wowote bila kujali kabila, dini wala tabaka.