Bingwa wa ndondi Conjestina Achieng azima uvumi kuwa ameaga dunia

Bondia huyo ameweka wazi kuwa yuko sawa na anaendelea vyema na matibabu.

Muhtasari

•Bingwa huyo wa ndondi amewasuta watu ambao walikuwa wakieneza uvumi kuwa amefariki baada ya afya yake kudhoofika.

•Conjestina alizungumza na waandishi wa habari baada ya kutembelewa na aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko.

katika hospitali ya Mombasa Women Empowerment Network Hospital huko Miritini siku ya Jumamosi, Septemba 3, 2022.
Bingwa wa ndondi Conjestina Achieng na gavana wa zamani wa Nairobi Mike Sonko katika hospitali ya Mombasa Women Empowerment Network Hospital huko Miritini siku ya Jumamosi, Septemba 3, 2022.
Image: ONYANGO OCHIENG'

Bondia wa zamani wa kimataifa wa Kenya Conjestina Achieng' amejitokeza na kuzizima tetesi kuwa ameaga dunia.

Akizungumza siku ya Jumamosi katika hospitali ya Mombaa Women Empowerment Network ambako amekuwa akihudumiwa, Conjestina aliweka wazi kuwa yuko sawa na anaendelea vyema na  matibabu.

"Mimi naendelea vizuri. Kila kitu kiko sawa. Naendelea na matibabu. Wale watu walikuwa wakisema eti nimekufa, sijafa niko sawa," aliwaambia wanahabari.

Bingwa huyo wa ndondi aliwasuta watu ambao walikuwa wakieneza uvumi kuwa amefariki baada ya afya yake kudhoofika.

Alisema kwa sasa yuko vizuri zaidi na hata anafanya mazoezi katika juhudi za kurejea kwenye ulingo wa ndondi hivi karibuni.

"Watu wajaribu kuchunga ulimi. Wakati wanaposema kitu wanafaa kujua maana yake kabla ya kusema," Alisema

Conjestina alizungumza na waandishi wa habari baada ya kutembelewa na aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko.

Mwanasiasa huyo alikuwa ameenda kumjulia hali Conjestina na kumpelekea vifaa vya kufanyia mazoezi ya ndondi.

"Nataka nitetee taji langu la  IBF . Wadhamini wakaingilia kati naweza kushukuru. Nimeanza mazoezi tayari," Conjestina alisema baada ya kupokea vifaa hivyo.

Uvumi ulianza kuenea kwenye mitandao ya kijamii tangu Alhamisi kwamba mwanabondia huyo ameaga dunia.

Conjestina alilazwa katika hospitalini mapema Julai baada ya afya yake na hali yake ya kiakili kuwa mbaya.