Johanna Ng'eno atimuliwa kama Mwenyekiti wa Kamati ya Makazi bungeni

Wakati wa upigaji kura, wanachama 12 kati ya 15 wa kamati hiyo walipiga kura ya kumuondoa Ng’eno.

Muhtasari

• Wanachama wa kamati hiyo walipiga kura ya kumwondoa Ng’eno kama Mwenyekiti kwa madai ya matumizi mabaya ya mamlaka yake. 

Mbunge wa Emurua Dikir Johana Ng'eno.
Mbunge wa Emurua Dikir Johana Ng'eno.
Image: Maktaba

Mbunge wa Emurua Dikirr Johanna Ng’eno amezingirwa kwa madai ya ufisadi na uzembe kama Mwenyekiti wa Kamati yenye ushawishi ya Makazi na Mipango ya Miji katika Bunge la Kitaifa.

Ng’eno ambaye alichaguliwa tena kwa tiketi ya UDA kwa muhula wa pili amekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Makazi na yenye ushawishi hadi wiki hii wakati wanachama wa kamati hiyo walipompiga kura kumtimua kutokana na tuhuma za ufisadi.

Wanachama wa kamati hiyo walipiga kura ya kumwondoa Ng’eno kama Mwenyekiti kwa madai ya matumizi mabaya ya mamlaka yake. 

Wakati wa upigaji kura, wanachama 12 kati ya 15 wa kamati hiyo walipiga kura ya kumuondoa Ng’eno. Wabunge pia walimkashifu Ng’eno kwa kuwatenga katika masuala muhimu, wakionya kuwa jambo hilo litakuwa hatari kwa mpango wa ujenzi wa nyumba ambao ni muhimu kwa utawala wa Rais William Ruto.

Wanakamati hao mnamo Jumanne walifanya vikaokadhaa na Spika Moses Wetangula kujadili mienendo ya mwenyekiti wao ambaye walimshutumu kwa kuendesha kamati hiyo pasi na kuhusisha wanachama wengine.

Mbunge huyo wa Emurua Dikirr, mshirika mkuu wa Rais Ruto na ambaye amechangia pakubwa kushinikiza kupitishwa kwa sheria ya Makazi ya bei nafuu katika Bunge la Kitaifa anakuwa mwenyekiti wa kwanza wa kamati kuondolewa katika wadhifa wake katika Bunge la 13.