Nairobi: Watu Zaidi ya 4,000 walilia haki Pasta akiwalaghai Zaidi ya Ksh 600M na kuingia mafichoni

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Zaidi ya Wakenya 4000 wamejitokeza na kusema kwamba Mhubiri huyo aliwalaghai pesa kati ya laki moja na laki moja na nusu akiwaahidi kuwa atawatafutia kazi ughaibuni.

Muhtasari

• Maafisa kutoka idara ya upelelezi DCI ilifika katika ofisi hiyo na kuwakamata baadhi ya wafanyikazi lakini mchungaji huyo hakupatikana kwani bado yuko mbioni.

Image: BBC

Polisi jijini Nairobi wanamsaka mhubiri mmoja baada ya watu Zaidi ya elfu 4 kujitokeza na kuandikisha ripoti kumtuhumu mhubiri huyo kwa kuwalaghai mamilioni ya pesa kwa ahadi hewa za kuwatafutia kazi nje ya nchi.

Kwa mujibu wa ripoti iliyopeperushwa kwenye runinga ya Citizen, mshukiwa huyo ambaye ni mchungaji wa kanisa moja anatuhumiwa kuwalaghai watu, idadi kubwa ikiwa ni waumini wa kanisa lake Zaidi ya shilingi milioni 600.

Mhubiri huyo ambaye alikuwa na ofisi yake katika jumba moja jijini kwa sasa yuko mafichoni.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Zaidi ya Wakenya 4000 wamejitokeza na kusema kwamba Mhubiri huyo aliwalaghai pesa kati ya laki moja na laki moja na nusu akiwaahidi kuwa atawatafutia kazi ughaibuni.

“Walikuwa wametuambia mchakato unachukua miezi 3, nimevumilia huo muda wote kutoka JUlai hadi Desemba halafu hawakuwa wananipigia, lazima mimi nije niwabembeleze na nilikuwa natoka mbali nalipa nauli nikifika huku waanza kuwa na kiburi hata hawaniangalilii mchakato na sasa wananiambia eti nimepigwa marufuku, hilo jambo limeniudhi sana na ningetaka haki itendeke turudishiwe pesa zetu,” mwanadada mmoja mwathirika wa ulaghai huo alisema.

Maafisa kutoka idara ya upelelezi DCI ilifika katika ofisi hiyo na kuwakamata baadhi ya wafanyikazi lakini mchungaji huyo hakupatikana kwani bado yuko mbioni.

Wengi wa waathirika wa ulaghai huo walisema kwamba baada ya kumaliza mchakato wa malipo, kampuni hiyo ya pasta haikuwa inawafuatilia hata kwa simu bali ilikuwa inawabidi wao tena kufanya marejeleo kufuatilia mchakato wao wa kusafiri nje ya nchi kikazi.

Waathirika wengi ni vijana waliomaliza shule hivi majuzi, idadi kubwa ikiwa ni waumini wa kanisa la mchungaji huyo lililoko Roysambu, viungani mwa jiji kuu la Nairobi.