Pastor Ezekiel aonya Wajaluo, Waluhya dhidi ya kununua majeneza ya kifahari

Mchungaji huyo alisema kusherehekea mauti ni kukaribisha roho ya umauti kurudi tena.

Muhtasari

• Kulingana naye, kufanya mazishi ya kifahari ni kukaribisha roho ya umauti kupiga hodi tena.

• Alisema inaporudi, inachukua mtu wa kutegemewa katika familia na kuacha wale wa hovyo.

mchungaji Ezekiel Odero
mchungaji Ezekiel Odero
Image: Facebook

Mchungaji Ezekiel Odero kwa mara nyingine ameibuka na mahubiri mengine ambayo yamezua mjadala mkali katika jamii haswa za Luo na Luhya magharibi mwa Kenya.

Katika video moja ambayo ilipakiwa TikTok, mchungaji Ezekiel alionya jamii hizo dhidi ya kuandaa hafla za mazishi za kifahari kwa kutumia gharama kubwa.

Kulingana naye, kununua majeneza na bei ghali yenye hadi ya nyota tano kwa ajili ya maiti na kupaisha mazishi ni sawa na kuvutia pepo ya mauti kupiga hodi mara kwa mara katika boma lenu.

Odero alitoa onyo kuwa hakuna haja ya kufanya mazishi kuwa ya kifahari kwani hivyo ni sawa na kufurahisha pepo ya mauti kutaka kuja tena na tena ili kusherehekea fahari hiyo.

“Na ukienda Ujaluoni, wanatengeneza majeneza ya pesa nyingi na makaburi yanaundwa mazuri. Na Magharibi hao ndio wanafanay mazishi hata na mifugo, kuingiza ng’ombe ndani ya nyumba hadi watoke ndio waingize maiti. Na ninawaonya, jinsi unavyotunza matanga, ndivyo roho ya mauti inapenda kwenu, roho ya mauti inasherehekea na itakula mtu mwingine” mchungaji Ezekiel Odero alitoa ilani.

Mchungaji huyo alizidi kutia woga kwa kusema roho hiyo ya umauti inapopiga hodi tena, huwa inachagua yule mtu tegemezi katika familia.

“Na roho ya mauti inapokuja, haitakula mtu mjinga, itachagua yule msomi mwenye pesa. Ukienda Ujaluoni unakuta kaburi la profesa, daktari.. watu wa maana tu. Halafu wale wanaobai ni wa kutembea kwenda nyuma na kuyumba kando kando kwa ulevi chakari,” Odero alisema.