Sonko asherehekea kutahiriwa kwa mtoto Satrine, aliyeponea kifo mamake akiuawa na Al Shabaab

Al Shabaab walishambulia kanisa la Joyland Likoni na kufyatua risasi kiholela ambapo waliua mama yake, risasi ambayo pia ilimjeruhi vibaya mtoto huyo kichwani.

Muhtasari

• Mwaka 2014, Al Shabaab walivamia kanisa Mombasa na kuua mama huyo akiwa ameshikilia mtoto mikononi.

• Risasi iliyomuua mama huyo ilipita kichwani mwa mtoto Satrine na kumuacha na majeraha mabaya.

• Sonko alijitolea kumuasili pamoja na nduguye mkubwa, Gift ambaye alimpakata nduguye huku akilia mbele ya mwili wa marehemu mama yao kanisani.

Mike Sonko akiwa na mtoto Satrine Osinya
Mike Sonko akiwa na mtoto Satrine Osinya
Image: Instagram

Mfanyibiashara na mwanasiasa maarufu Mike Sonko amefurahia baada ya mtoto Satrine Osinya kupitia mila ya kiafrika ya kutahiri kama njia moja ya kuonesha kuvuka kutoka utoto hadi utu uzima.

Kwa wale wasiojua, Satrine ni mtoto ambaye Sonko aliamua kumuasili baada ya mamake kupigwa risasi na kufa akiwa kanisani naye, kipindi hicho mtoto huyo alikuwa na mwaka mmoja na nusu na alikuwa ubavuni mwa mamake wakati majambazi wanaokisiwa kuwa wanamgambo wa Al Shabaab walipovamia kanisa la Joyland huko Likoni na kuuwa makumi ya waumini.

Satrine na ndugu yake mkubwa, Gift Osinya walikuwa na mama yao kanisani humo na walishuhudia jinsi mama yao alimiminiwa risasi kadhaa hadi kufa mbele ya madhabahu.

Hadithi yao iligonga vichwa vya habari ambapo Sonko kwa moyo wake wa kujitoa kwa watu alijitolea kuwaasili watoto hao wawili na hata kuwahudumiwa kwa matibabu kutokana na majeraha ya risasi ambayo pia walipata katika shambulio hilo lililoghariu maisha ya mama yao.

Sonko alimtembelea katika kituo cha kutahiri ambapo walitahiriwa na watoto rika lake siku kadhaa zilizopita na hakusita kuonesha furaha yake kwa kumsherehekea malaika huyo ambaye alimsaidia na kumfanya kuwa mmoja wa familia yake pana.

“Leo mimi ni baba mwenye fahari sana baada ya kumtembelea mwanangu wa kuasili Satrin Osinya pamoja na wanarika wake wengine katika kanisa la PCEA Evergreen ambapo wanapona baada ya Kutahiriwa siku kadhaa zilizopita. Sasa zinabadilishwa kuwa watu wazima kupitia desturi yetu ya kutoka utoto hadi utu uzima. Pia tulitangamana na kusherehekea na watu wengine wa baba, wajomba na walezi wa kiume ambao pia walikuwa wamekuja kuwatembelea wana wao. Karibu katika utu uzima na kumbuka daima kuwa kama familia tunakupenda sana” Sonko aliandika.

Kwa upande wake, mkewe Sonko, Primrose Mbuvi alimsherehekea mtoto huyo akisema kuwa ana furaha hatimaye amemuona akiwa mtu mzima.

“Namshukuru Mungu, Mwanangu amekuwa mtu mwenye hekima na nguvu zaidi 🙏. Hongera sana Mtoto wangu wa kiume kwa ibada zako za kupita 👏👏 Nakuombea uwe salama na hodari daima 💪 ufurahie safari na usisahau kuwa siku zote nitakupenda mwanangu,” mkewe Sonko aliandika.