Mudavadi asema upinzani ni ardhi isiyo na rutuba, awarai Waluhya kumtema Odinga

Mku huyo wa baraza la mawaziri aliwataka Waluhya kuasi upinzani na kujiunga na serikali ili kupata mapochopocho.

Muhtasari

• Wakati ardhi yako haina rutuba na haizai matunda yoyote kila msimu, unaacha na kutafuta mashamba mengine yanayolimwa - Mudavadi.

Mudavadi awarai Waluhya kumtema Odinga
Mudavadi awarai Waluhya kumtema Odinga
Image: Maktaba

Mkuu wa baraza la mawaziri Musalia Mudavadi amewarai wanajamii yake kutoka kaunti ya Vihiga kuasi kabisa mrengo wa upinzani unaoongozwa na kinara wa Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga na badala yake kujiunga na mrengo wa serikali ya Kenya Kwanza unaoongozwa na rais William Ruto.

Akizungumza katika kaunti ya Vihiga alipohudhuria sherehe za tamaduni ya Wamaragoli ambao ndio wengi wa wakaazi wa kaunti hiyo, Mudavadi alisema kuwa jamii hiyo imekuwa katika uoinzani kwa muda mrefu na ni wakati sasa wafunguke macho na kuingia ndani ya serikali.

Alisema kuwa upinzani ni kiangazi na ukame ambao hauna mafanikio kwa jamii hiyo, hivyo kuwarai kuasi mrengo huo na kuingia ndani ya serikali ambako kulingana na yeye kuna chemchemi nzuri na mapochopocho mengi yatokanayo na kuwa ndani ya serikali inayoongoza taifa.

“Wakati ardhi yako haina rutuba na haizai matunda yoyote kila msimu, unaacha na kutafuta mashamba mengine yanayolimwa,” Mudavadi alisema akiwarai kumtema bwana Odinga ambaye kwa muda mrefu ukanda wa Nyanza na Magharibi mwa Kenya zimekuwa nguzo zake kisiasa.

Mudavadi alikuwa ni rafiki wa muda mrefu wa Odinga tangu uchaguzi wa mwaka 2017 ambapo pamoja waliasisi jina la muungano wa NASA ambao uliwania urais bila mafanikio.

Katika uchaguzi wa mwaka 2022, Mudavadi na mwenzake Moses Wetang’ula ambaye kwa sasa ni spika wa bunge la kitaifa walimkimbia Odinga na kujiunga katika kambi ya Ruto ambaye aliibuka mshindi wa uchaguzi wa urais na kuwatunuku nyadhifa za kumezewa mate kama Mkuu wa baraza la mawaziri na spika wa bunge la kitaifa mtawalia.