Odinga atetea Tuju na Salat kutembelea Cherera na wenzake baada ya kukataa matokeo

Odinga alisema wawili hao walikuwa wanafuatilia ukweli kwani tayari matokeo yalikuwa yametangazwa na Chebukati.

Muhtasari

• Pia Odinga alisisitiza kuwa kamati ya uchunguzi inawahukumu bure Cherera na wenzake na hawana hatia.

KINARA WA AZIMIO RAILA ODINGA AKIWAHUTUBIA WANAHABARI 3/11/2022
Image: ENOS TECHE

Kinara wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga ametetea hatua ya baadhi ya wanachama wa muungano huo kutembelea makamishna 4 wa IEBC walioasi matokeo ya uchaguzi wa urais.

Akizungumza katika mahojiano na runinga ya Citizen, Odinga alisema kuwa wakati Raphael Tuju na Nick Salat waliwatembelea Cherera na wenzake katika moja ya mgahawa ulioko maeneo ya Yaya jijini Nairobi, tayari matokeo yalikuwa yametangazwa na hao walikuwa wameyakataa.

Alisema ziara hiyo haikuwa na nia mbaya kwani ndio walikuwa wanafuatilia ili kujua ukweli wa maneno kuhusu ni kwa nini walipinga matokeo ambayo tangu mwanzo walikuwa wanayatoa kwa umma.

“Wanasiasa walikuwa na haki ya kuwatembelea makamishna hawa kwa sababu walikuwa wanasema ‘Hapana’ (kwa matokeo). Watu wetu walikuwa na haki ya kupata ukweli, kwa sababu hiyo ilikuwa tayari matukio ya baada ya uchaguzi. Matokeo yalikuwa tayari yametangazwa na Bw Chebukati,” Odinga alisema.

Makamishna Juliana Cherera, Irene Masit, Francis Wanderi na Justus Nyang’aya walijitenga na matokeo yaliyotangazwa na mwenyekiti Wafula Chebukati na kamati ya uchunguzi iliarifiwa kuwa baada ya kuondoka kituo kikuu cha uhesabu wa kura huko Bomas, walielekea katika mgahawa mmoja mtaa wa Kilimani ambapo baadhi ya wandani kutoka mrengo wa upinzani waliwatembelea kisiri.

Baada ya rais Ruto kuwasimamisha kazi wane hao ili kupisha uchunguzi kufanyika, tayari watatu kati yao wameshajiuzulu lakini Irene Masit angali bado kung’atuka ofisini.