Nyanyake Jeff Mwathi amlaani DJ Fatxo kuhusiana na kifo cha mjukuu wake

"Kila anapooga nataka awe anaona damu ya Jeff," Nyanyake Jeff alisema.

Muhtasari

•Nyanyake Mwathi alisema alishuku kuwa DJ Fatxo alikuwa akihongana ili asihusishwe na mauaji ya kijana huyo wa miaka 23.

•Alisisitiza kuwa DJ Fatxo alimuua marehemu huku akidai kwamba anaweza kuwa alifanya hivyo kwa madhumuni ya ushirikina.

Mwimbaji DJ Fatxo na marehemu Jeff Mwathi
Image: HISANI

Nyanya ya marehemu Jeff Mwathi amekashifu ucheleweshaji wa haki kupatikana katika kesi ya mauaji ya mjukuu wake.

Anasema hamu yake kubwa ni haki ya mjukuu huyo wake aliyeaga mwezi Februari kupatikana.

Akizungumza wakati wa mahojiano kwenye kituo cha YouTube cha Nakuru Leo, nyanyake Mwathi alisema alishuku kuwa DJ Fatxo alikuwa akihongana ili asihusishwe na mauaji ya kijana huyo wa miaka 23.

"Ninasihi ikiwa anaweza kuondolewa kutoka kwa watu wengine. Anajisifu kwa kuwa ana pesa lakini hamjui Mungu. Sijui kama alihongana au la. Kwa kweli, mambo yanafanyika gizani, ni dhahiri kuna kitu kinaendelea."

Bibi huyo alisisitiza kuwa DJ Fatxo alimuua marehemu huku akidai kwamba anaweza kuwa alifanya hivyo kwa ma ushirikina.

"Binadamu anagharimu kiasi gani?" Alihoji.

Nyanyake Mwathi aliongeza kuwa mwanamuziki huyo alipiga picha za marehemu akiwa amefungwa na kuzituma kwa watu kadhaa kabla ya mjukuu wake kutupwa nje ya nyumba yake.

Maneno yake ya mwisho kwa Fatxo? "Juzi nilisikia anataka kuenda nje ya nchi. Niliwaambia watoto wangu wamwache aende zake, Anaweza kuepuka sheria lakini hawezi kumkwepa Mungu. Popote atakapokwenda, damu ya Jeff itamfuata. Atakuwa akimuona Jeff wakati wowote anapotembea. Namwambia Jeff asilale. Nikamwambia Jeff amuulize kwanini alimuua. Kila anapooga nataka awe anaona damu ya Jeff. Ninamwomba Mungu kwamba popote Fatxo aendako aandamwe na Jeff." Alisema.