Ruto ampiku Odinga kwa umaarufu Magharibi mwa Kenya - TIFA

UDA ni maarufu zaidi ukanda wa Magharibi kwa 32% huku ODM wakitupwa hadi nafasi ya pili kwa 25%.

Muhtasari

• UDA hivi majuzi kilizindua ofisi zao mpya katika kaunti ya Kisumu.

• Katika uliokuwa mkoa wa Nyanza, UDA kimeongeza umaarufu hadi 23% huku ODM kikisalia chama maarufu kwa 63%.

Odinga akiwa na huzuni
Odinga akiwa na huzuni
Image: Maktaba

Chama kichanga cha UDA kinachoongozwa na rais William Ruto kina umaarufu mkubwa katika ukanda wa magharibi mwa Kenya kuliko kile kikongwe cha ODM kinachoongozwa na Raila Odinga.

Katika utafiti wa mwezi Machi uliofanywa na kampuni ya TIFA, UDA cha Ruto kimejizolea umaarufu kwa asilimia 32 huku ODM kikiwa cha pili kwa umaarufu kwa asilimia 25.

Ukanda wa Magharibi mwa Kenya katika miaka ya nyuma ulikuwa ukijulikana kuwa ngome ya kisiasa ya kinara wa Azimio Raila Odinga huku umaarufu wa chama chake cha ODM ukiwa juu Zaidi ya chama kingine chochote.

Lakini chini ya miaka mitatu tangu Ruto kizundua chama cha UDA kwa wafuasi wake akilenga kumrithi aliyekuwa rais Kenyatta, chama hicho kimechukua mizizi katika maeneo mengi yaliyokuwa yakitawaliwa na ODM.

Katika umaarufu wa vyama ukanda wa magharibi, chama cha spika wa bunge la kitaifa Moses Wetang’ula FORD-K ni cha tatu kwa umaarufu kwa asilimia 9 huku chama cha aliyekuwa waziri wa ulinzi Eugine Wamalwa DAP-K kikifunga nne bora na 4%.

Katika ngome nyingine ya kisiasa ya Raila Odinga, Nyanza, chama cha UDA japo hakijakipiku kile cha ODM kimepata umaarufu mkubwa huku sasa kikiwa cha pili.

Ukanda wa Nyanza ambapo ndiko nyumbani kwa Odinga, ODM ni maarufu kwa 63%, UDA cha Ruto ambacho hivi majuzi kimezindua ofisi yao Kisumu kikiwa cha pili kwa 23% na Jubilee kikiwa na umaarufu finyu wa 2%.

Ukanda wa mlima Kenya, North Rift, Kaskazini mwa Kenya, UDA kina umaarufu mkubwa huku ODM nacho kiking’ra Nairobi, South Rift, Pwani, Lower Eastern na Nyanza.