Rais William Ruto: Hakuna kitu kama ofisi ya binti wa rais, ni mzaha tu!

Ruto alisisitiza kwamba hakuna mtu wa familia yake anafaa kujihusisha katika siasa na hawezi tumia nafasi ya urais kuwapandisha wanafamilia kwenye siasa.

Muhtasari

• "Na nilimwambia Charlene Kwamba watu wengi wataielewa vibaya lakini aliniambia kuwa hivyo ndivyo ameamua kujiita.”

• Ruto alisisitiza kwamba binti yake Charlene hafai kuhusishwa katika siasa kwa njia yoyote kwani yeye si mwanasiasa.

Rais Ruto amtetea bintiye Charlene Ruto
Rais Ruto amtetea bintiye Charlene Ruto
Image: Facebook

Rais William Ruto kwa mara nyingine tena amezungumzia ofisi ya binti wa kwanza wa taifa – ambayo ilizinduliwa na bintiye Charlene Ruto miezi kadhaa iliyopita.

Ruto akilijibu swali la mkwasi Mo Ibrahim katika ukumbi wa KICC ambaye alikuwa anataka kujua ofisi ya binti wa kwanza wa taifa ni nini, kiongozi wa taifa alisema kuwa hakuna ofisi kama hiyo huku akiitaja kama mzaha wa Kenya tu ambao ulianzishwa na Charlene kweney ukurasa wake wa Twitter kama njia moja ya kutofautisha akaunti yake na zile ghushi.

Rais alisisitiza kwamba watu wa familia yake hawafai kujihusisha katika siasa hata kidogo.

“Nafikiri Mo unaniingilia sana,” Ruto alianza kujibu kwa mzaha huku wote wakicheka. “Ni mzaha wa Kenya tu kwa sababu binti wangu asiye na hatia Charlene aliiweka kwenye akaunti yake ya Twitter na nilimuuliza mbona umefanya hivi akanijibu kuwa ni kutofautisha akaunti halali na zile ghushi. Na nilimwambia Kwamba watu wengi wataielewa vibaya lakini aliniambia kuwa hivyo ndivyo ameamua kujiita.”

Kongozi wa taifa alisisitiza kwamba hana nia ya kufadhili ofisi ya binti wa kwanza kwa kutumia ushuru wa wananchi huku akisema kuwa filosofia yake ya uongozi inaamini Zaidi kwamba kila kitu hakifai kuzunguka katika rais. Alisema kuwa Wakenya wamesonga mbele na hilo.

“Ukiangalia katika jinsi naangalia jinsi nchi tunafaa kusonga mbele, maendeleo ya kujumuisha kila mtu, filosofia yangu inasema kwamba kila kitu hakifai kuzunguka katika urais, hata kama ni William Ruto. Watu wa familia yangu hawafai kujihusisha katika siasa, lakini sisemi kwamba hawapaswi, kama watataka hilo ni lao lakini mimi nasema inatosha kwamba wakenya wamenipa heshima ya kuwa rais wao na sifai kutumia nafasi hiyo kupaisha familia yangu kwenye siasa,” rais Ruto alisema.

Ruto alisema kuwa nafasi aliyopewa na wakenya kama rais ni kuitumia kupaisha na kuinua watoto wa watu wengine ili wapate nafasi kama zile ambazo yeye amepata.