Nairobi: Mwenye digrii ya uzamili aishtaki kampuni kwa kumshrutisha kulea watoto wa bosi

“Mhojiwa wa 1 amempa mlalamishi kazi ya kiwango cha chini isiyohusiana na maelezo ya kazi yake, uzoefu na uwezo wake ambao umeishia kuchukua nafasi yake katika shirika" - hati ya mahakama.

Muhtasari

• Mrembo huyo mlalamikaji ana Shahada ya Uzamili ya Utawala wa Biashara (Usimamizi wa Rasilimali Watu).

Mahakama ya Milimani mjini Nairobi
Mahakama ya Milimani mjini Nairobi

Kizaazaa kilishuhudiwa katika mahakama ya uajiri la leba jijini Nairobi baada ya mrembo mmoja kuipeleka mahakamani kampuni moja isiyo ya kiserikali kwa kile alisema kuwa ilimpa kazi ya kuwalea watoto wa bosi wao kama ajira licha ya kuwa na masomo hadi kiwango cha uzamili.

Katika hati za malalamishi za mrembo huo, sasa anaitaka kampuni hiyo kumpa malimbikizi ya shilingi milioni 32 pesa za Kenya kwa kile alisema kuwa alikosewa heshima kupewa kazi isiyoambatana na maelezo ya vyeti vyake.

“Mhojiwa wa 1 amempa mlalamishi kazi ya kiwango cha chini isiyohusiana na maelezo ya kazi yake, uzoefu na uwezo wake ambao umeishia kuchukua nafasi yake katika shirika. Kwa mfano, mlalamishi amelazimika kulea watoto wa mtangulizi wa mjibu maombi wa pili wakati wa safari yake kwenda Arlington kwa mkutano wa viongozi mnamo Januari 2020," sehemu ya hati za korti ilisoma.

Ingawa mrembo huyo mlalamikaji ana Shahada ya Uzamili ya Utawala wa Biashara (Usimamizi wa Rasilimali Watu) na Mtaalamu aliyeidhinishwa wa Rasilimali Watu, alisema kuwa alilazimika kufanya kazi ya kuwalea watoto.

Hati zilizowasilishwa mahakamani zinaonyesha kuwa mnamo au karibu Januari 26, 2016, mlalamikaji aliajiriwa kama Msaidizi Mtendaji wa Nafasi ya Makamu wa Rais Mwandamizi wa kampuni hiyo.