Wavulana 4 wambaka msichana katika choo cha kanisa usiku na kutiririsha video TikTok

Wavulana hao wote wana umri wa miaka 17 na walimfungia msichana wa miaka 16 kwenye choo cha kanisa na kumbaka usiku kucha huku video hiyo wakiwa wanaitiririsha moja kwa moja TikTok.

Muhtasari

• Washukiwa hao ambao wote ni wanafunzi, wanaishi na wazazi wao.

• Wanashtakiwa kwa kula njama, ubakaji na unyanyasaji mtandaoni.

Mhasiriwa wa dhuluma za kijinsia
GBV: Mhasiriwa wa dhuluma za kijinsia
Image: THE STAR

Mahakama moja nchini Nigeria ilibung’aa baada ya kisa cha kughadhabishwa kusimuliwa mbele yao kuhusu wavulana wanne wenye umri wa miaka 17 walioshirikiana na kumbaka msichana wa miaka 16 kwa zamu katika choo cha kanisa usiku kucha.

Kwa mujibu wa habari za kituo cha runinga nchini humo, wavulana hao walimvizia msichana huyo katika choo cha kanisa usiku wakati wa ibada ya kesha na kumfanyia kitendo hicho hadi asubuhi huku wakitiririsha video hiyo moja kwa moja kwenye mitandao ya TikTok na WhatsApp, mahakama iliambiwa.

Mahakama iliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 2, 2023, ikisubiri ushauri kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka wa Jimbo la Ogun.

Kulingana na Shirika la Habari la Nigeria, vijana hao watawekwa chini ya ulinzi wa Kituo cha Marekebisho hadi tarehe inayofuata ya kusikilizwa.

Washukiwa hao ambao wote ni wanafunzi, wanaishi na wazazi wao katika eneo la Ikosi Ketu, Jimbo la Lagos. Wanashtakiwa kwa kula njama, ubakaji na unyanyasaji mtandaoni.

Hakimu hakukubali maombi yao kabla ya kuwarejesha rumande na kuahirisha kesi hiyo.

Haya yanaripotiwa wakati humu nchini vijana wengi ambao ni watumizi wa mtandao wa video fupi TikTok wakituhumiwa kwa kugeuza mtandao huo kuwa ulingo wa anasa na usherati nyakati za usiku.

Inaarifiwa kwamba vijana hao hutiririsha video zao moja kwa moja nyakati za usiku wakifanya vitendo vya anasa, na hivyo kuchafua mantiki na dhumni la mtandao huo unaomilikiwa na kampuni ya Uchina ambao ulinuia kusisimua na kufurahisha watu kwa video fupi za kuchekesha na pia kujifunza.