Nairobi: Mchuuzi wa mayai, smokie na kachumbari ahesabu hasara baada ya uvamizi wa kanjo

“Leo baba mtu, mwana, kaka, mama, dada analala njaa, labda kafungiwa na mwenye nyumba, labda kesho watoto wao wasiruhusiwe kuhudhuria masomo kwa sababu ya uovu huu wa kinyama," mmoja alisema.

Muhtasari

• Toroli lenye smokie, mayai na kachumbari lilionekana limevunjwa na katika picha nyingine lilirushwa ndani ya lori la kanju huku baadhi ya mayai na smokie zikisalia kutawanyika sakafuni.

Mchuuzi wa mayai na kachumbari ahesabu hasara Kanju wakivamia.
Mchuuzi wa mayai na kachumbari ahesabu hasara Kanju wakivamia.
Image: Facebook

Wakenya kwenye mitandao ya kijamii wameonesha kukerwa kwao na picha ambazo zimekuwa zikisambazwa zikionesha mtaji wa mchuuzi wa vyakula kando ya barabara jijini Nairobi kuharibiwa na watu wanaoshukiwa kuwa askari wa kaunti maarufu Kanju.

Katika picha hizo za kuvunja moyo, trolley ya kuchuuzia vyakula vidogo vidogo kama smokie, sambusa, na kachumbari vyote vilionekana vimetawanyika kwenye sakafu ya lami.

Wakenya walimhurumia mchuuzi huyo ambaye pengine alikuwa ndiye tegemeo la pekee katika nyumba yake na aliyetegemewa pengine jioni kurudi kwa nyumba na pakiti ya unga wakati huu uchumi unaendelea kuwakereketa wengi wa Wakenya kutoka matabaka yote ya maisha.

Baadhi ya Wakenya walimshtumu gavana wa Nairobi Johnson Sakaja kwa uovu huo huku wengine wakijitolea kumnunulia mtaji mchuuzi huyo ili kujikusanya na kujijenga upya baada ya kile kinachonekana kama kuzimiwa mwanga katika maisha yake ya kibiashara ghafla.

“Sakaja Johnson hii haistahili kabisa kwa bwana Gavana! Je, Serikali ya Kaunti haiwezi kutenga nafasi kwa wachuuzi hawa wa vyakula badala ya kuwadhulumu hivi? Hapa umekosea hustlers!” mmoja alisema.

“Leo baba mtu, mwana, kaka, mama, dada analala njaa, labda kafungiwa na mwenye nyumba, labda kesho watoto wao wasiruhusiwe kuhudhuria masomo kwa sababu ya malimbikizo ya ada, labda wazee wanaowategemea wakashindwa kupata vidonge vya shinikizo na kisukari… kwa sababu ya uovu huu kwa waliyemtegemea,” mwingine alimhurumia.

“Mtu fulani ameahidi kusaidia kuhifadhi tena chochote kilichokuwa kwenye toroli ikiwa tunaweza kumtafuta mmiliki. Unajua tunawezaje kumfikia ndio watoto wasilale njaa?,” mwingine pia aliuliza kuelekezwa kwa mchuuzi huyo ambaye kwa dalili zote aliko Analia kwa uchungu.