Sonko akutana na mwanamke ambaye picha yake ilihaririwa kuonekana chafu , achukua hatua muhimu

Gavana huyo wa zamani alishiriki mazungumzo na mwanamke huyo na hata kupanga vikao vya ushauri kwa ajili yake.

Muhtasari

•Sonko alikutana na mwanamke aliyeketi nyuma yake wakati wa hafla ya ukoo wa Anzauni, katika kaunti ya Kitui takriban wiki moja iliyopita.

•Sonko alipanga vikao vya ushauri kwa ajili ya mwanamke huyo ili aweze kukabiliana na kiwewe kilichotokana na uhariri huo.

Aliyekuwa gavana wa Nairoi, Mike Sonko
Aliyekuwa gavana wa Nairoi, Mike Sonko
Image: Facebook//Mike Sonko

Siku ya Jumanne, aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Mbuvi Sonko alikutana na mwanamke aliyeketi nyuma yake wakati wa hafla ya ukoo wa Anzauni, katika kaunti ya Kitui takriban wiki moja iliyopita.

Hii ni baada ya picha iliyochapishwa na mwanasiasa huyo ikimuonyesha yeye na mwanamke huyo nyuma yake kuwavutia wanamitandao watukutu ambao waliihariri ili kuifanya ionekane chafu.

Katika taarifa yake ya Jumanne jioni, mfanyibiashara huyo tajiri alifichua kuwa alishiriki mazungumzo na mwanamke mwathiriwa na hata kupanga vikao vya ushauri kwa ajili yake ili kuweza kukabiliana na kiwewe kilichotokana na uhariri huo.

"Kwa sasa niko na mwanamke wa R*sec*c* aliyefanyiwa photoshop katika afisi zangu za Upperhill tukipanga vikao vya ushauri," Mike Sonko alisema kupitia Twitter.

Aliongeza, “Kwa sababu za faragha, sitafichua utambulisho wake au kushiriki picha na video za mkutano huo kwa sababu ya heshima niliyo nayo kwa wanawake. Tujenge utamaduni wa kuwalinda wanawake wetu katika jamii dhidi ya udhalilishaji huo.

Wikendi ya wiki jana, wanamitandao walizua minong’ono baada ya picha kuvujishwa kutoka kwa hafla ya jamii ya Anzauni kaunti ya Kitui ambayo gavana wa zamani wa Nairobi Mike Sonko alihudhuria kama mmoja wa wageni waalikwa.

Katika picha hiyo iliyoenezwa pakubwa mitandaoni, Sonko alionekana ameketi akiwa nadhifu kama kawaida yake lakini nyuma yake, pembeni kushoto palionekana mwanamke ambaye alionekana kuwa na sketi fupi.

Picha hiyo kwa bahati mbaya ilifanyiwa uhariri na hiyo kuzua gumzo kubwa mitandaoni baadhi wakienda mbali zaidi na kutoa ufafanuzi wa kina kana kwamba ni VAR inayochunguza madhambi ya wanasoka uwanjani.

Sonko aligutushwa na hilo na baadae katika mtandao wa X alichapisha mfululizo wa picha halisi ambazo alisema kuwa ni ‘VAR ya ukweli’ na kusema kwamba picha hiyo ilikuwa imehaririwa ili kumuonesha mwanamke wa watu kuwa alikuwa ‘bila’.

“Baada ya uchunguzi wa kina na kupitia picha asili zilizochukuliwa wakati wa hafla ya jamii ya Anzauni huko Kitui wikendi iliyopita ambapo nilikuwa mmoja wa wageni waalikwa, nimekuja kubaini kwamba picha inayodaiwa kuwa ya mwanamke nyuma yangu anayeonekana kuweka wazi nyeti zake si ya kweli, imehaririwa,” Sonko alisema kwa sehemu.

“Picha hiyo imehaririwa ili kuibua dhana kwamba ‘rosecoco’ ya mwanamke huyo inaonekana, ambapo si kweli,” aliongeza.

Kiongozi huyo wa zamani wa Nairobi alifichua kwamba kiti hicho kilikuwa kimehifadhiwa kwa ajili ya waziri Penina Malonza lakini wanawake mbalimbali walikikalia kwa muda tofauti tofauti akisubiriwa waziri huyo kufika.

Sonko alituhumu vikali yeyote ambaye alihusika katika kuhariri picha hiyo ili kuonesha kwamba mwanamke huyo alikuwa ‘bila’ na kusema kwamba ni mama ya watu ambaye ameathirika kwa njia hasi kutokana na picha hiyo kuenezwa.

“Hata kama mwanamke huyo simjui, sio tu kwamba yeye ni uso miongoni mwa umati bali pia ni mama ya watu, shangazi, binti au hata dada wa watu. Anastahili heshima. Kwa hivyo, ninatoa wito kwa yeyote ambaye anamfahamu kumjulisha kwamba ninamtafuta ilia je kwa ofisi yangu tuanzishe mkakati wa kuwatafutia huduma za ushauri nasaha pamoja na familia yake,” Sonko alitoa ombi.