Mzazi alilia haki mwanawe wa miaka 11 akifariki shuleni katika mazingira tatanishi

Mvulana huyo alitoweka Jumanne jioni wakati babake alikwenda kumchukua kutoka shuleni na baada ya msako, mwili wake ulipatikana ndani ya bwawa la shule Jumatano asubuhi.

Muhtasari

• Familia hiyo inaulaumu uongozi wa shule kwa kuzembea kazini mwao na kutaka uchunguzi Zaidi kufanyika ili marehemu mwanao apate haki.

Mwanafunzi aliyefariki shuleni
Mwanafunzi aliyefariki shuleni
Image: Screngrab//CITIZEN TV

Familia ya mtoto wa miaka 11 aliyefariki wakati anaogelea katika bwawa la shule mtaani Parklands inadai haki.

Marehemu Iilyaas Abdikarim Ali Mohamud, mvulana mwenye umri wa miaka 11 ambaye alikuwa mwanafunzi katika shule ya msingi ya Visa Oshwal mtaani Parklands aliripotiwa kutoweka Jumanne alasiri wakati babake alikwenda kumchukua kutoka shuleni baada ya masomo ya siku kukamilika.

Hata hivyo, mzazi alipofika shuleni, mwanawe hakuweza kupatikana na hilo lilizua tumbojoto kupelekea msako ambapo mtoto huyo alipatikana amefariki ndani ya bwawa la shule Jumatano asubuhi.

Polisi katika eneo la Parklands na maafisa wa Wizara ya Elimu wameanzisha uchunguzi kuhusu tukio hilo.

Mamake Abdikarim ambaye alizungumza na Citizen TV alionekana kutofarijika kwani habari za kifo cha mwanawe shuleni zilikuwa nzito sana kustahimili.

Familia ilisema mwanafunzi huyo wa Darasa la Pili alitoweka Jumanne alasiri na baba alijua kuhusu hilo mwendo wa saa kumi jioni alipoenda kumchukua kutoka shuleni. Juhudi za kumtafuta hazikufua dafu.

"Sasa mimi niliuliza kila pahali tunaangalia hakuna nimekosa sasa kocha huyo nimemuuliza alafu anasema hii ni darasa gani nikamwambia Grade 2. Faith akaleta karatasi na akasema kuwa darasa lao leo hawana swimming," baba alisema.

Familia hiyo inaulaumu uongozi wa shule kwa kuzembea kazini mwao na kutaka uchunguzi Zaidi kufanyika ili marehemu mwanao apate haki.

"Tunaona kuna uzembe mkubwa sana ulifanywa kwa mfano kama mtoto ametoka darasa na saa moja mtoto hajarudi kwa darasa hilo mwalimu hakuwa na shaka huyu mtoto pengine kuna kitu fulani kilichofanyika...hiyo ni jambo moja ambalo hatuwezi kuvumilia," Mohamed Adan, mwanafamilia mwingine aliesema kwa ghadhabu.