Sonko afichua kwa nini anataka kumhamisha Kimani Mbugua kutoka Mathare hadi rehab ya Mombasa

Alifichua kwamba alipata kumuona Kimani Mbugua, akazungumza naye na kushiriki naye wakati mzuri.

Muhtasari

•Sonko alifichua kuwa madhumuni ya ziara yake ilikuwa kuangalia maendeleo ya Kimani na mwanahabari wa zamani wa NTV Eunice Omollo.

•Sonko alisisitiza kuhusu mpango wake wa kumhamisha Kimani ambaye amekuwa akikabiliana kutoka Mathare hadi Mombasa.

walimtembelea Kimani Mbugua katika hospitali ya Mathare.
Mike Sonko na Oga Obinna walimtembelea Kimani Mbugua katika hospitali ya Mathare.
Image: TWITTER// MIKE SONKO

Siku ya Jumatano, aliyekuwa gavana wa kaunti ya Nairobi Mike Sonko alimtembelea aliyekuwa mwanahabari wa Citizen TV Kimani Mbugua katika hospitali ya Mathare ambako amelazwa kwa sasa.

Katika taarifa yake ya Alhamisi asubuhi, mfanyabiashara huyo mbwenyenye alifichua kuwa madhumuni ya ziara yake ilikuwa kuangalia maendeleo ya Kimani Mbugua na mwanahabari wa zamani wa NTV Eunice Omollo.

Alifichua kwamba alipata kumuona Kimani Mbugua, akazungumza naye na kushiriki naye wakati mzuri.

“Nilitembelea hospitali ya Mathare pamoja na Oga Obbina na familia ya Kimani Mbugua ili kuangalia maendeleo yao (Kimani na Omollo)  ya kupata nafuu. Tulikaribishwa kwa moyo mkunjufu na timu ya madaktari waliokuwa wakiwasimamia ambao walitufahamisha maendeleo yao. Hata hivyo, Eunice Omollo alikuwa chini ya matibabu katika wadi ya wanawake tulipozuru, nilipata nafasi ya kutangamana na Kimani Mbugua pekee. Tulikuwa na wakati mzuri pamoja na Kimani Mbugua tukileta kumbukumbu za mahojiano ya zamani na mjadala mpana wa mapambano yake ya sasa,” Sonko alisema kupitia Twitter.

Gavana huyo wa zamani aliambatanisha taarifa yake na video yake akiwa katika Hospitali ya Mathare ambapo alikuwa na mawasiliano mazuri na mwanahabari Kimani Mbugua.

Sonko alisisitiza kuhusu mpango wake wa kumhamisha mwanahabari huyo kijana ambaye amekuwa akikabiliana na masuala ya kiakili kutoka Mathare hadi kwa kituo cha marekebisho ya tabia cha Hospitali ya Wanawake ya Mombasa akisema kuwa mabadiliko ya mazingira yatamsaidia katika mchakato wa kupona.

"Kimani mbugua tayari ametoa mengi kwa ulimwengu kupitia kazi yake, na ni wakati wetu wa kurudisha matumaini, upendo na utunzaji. Tulivutiwa sana na huduma za uongozi mzima wa hospitali hiyo, ni hospitali nzuri sana yenye wahudumu wa afya waliohitimu na kitaaluma.  Kwa hiyo hata kama tutawahamishia Mombasa itakuwa tu kwa malengo ya kubadilisha mazingira ambayo yanaweza pia kuchangia pakubwa kupona kwa mgonjwa na ndiyo maana niliamua pamoja na familia kuwahamishia Mombasa Women Rehabilitation Center ambapo Conjestina Achieng yuko tuone kama watachange for good,” alisema.

Mwanasiasa huyo aliyezingirwa na utata alikariri kuwasapoti Kimani na Bi Omollo katika safari yao ya kupona na kuwatakia afueni ya haraka.