Wafungwe maisha! Millie Odhiambo akerwa na wanaorekodi na kusambaza matukio ya kitandani

Odhiambo alitaka sheria ifanyiwe marekebisho naadhabu kali zitolewe kwa wanaosambaza picha chafu za wanawake.

Muhtasari

•Akizungumza katika kikao cha bunge, Bi Odhiambo aliwataka DCI kujitahidi kuwakamata watu wanaojihusisha na vitendo kama hivyo.

•Alisema kkuwa watu wanapaswa kuzingatia madhara ya vitendo vyao kabla ya kuchukua hatua ya kusambaza picha kama hizo.

Image: MAKTABA

Mbunge wa Suba Kaskazini Millie Odhiambo Mabona ametoa onyo kali kwa wanaume wanaosambaza picha chafu za wanawake.

Akizungumza wakati wa kikao cha bunge, Bi Odhiambo aliwataka DCI kujitahidi kuwakamata watu wanaojihusisha na vitendo kama hivyo.

Odhiambo ambaye alisema amekerwa sana na kisa cha hivi majuzi ambacho kilimhusisha CAS Millicent Omanga alitaka sheria ifanyiwe marekebisho ambapo adhabu kali zitatolewa kwa watu wanaosambaza picha chafu za wanawake.

"Siungi mkono hukumu ya kifo, lakini natamani ningefanya hivyo. Kama ningekuwa naunga mkono hukumu ya kifo, ningeunga mkono hukumu ya kifo kwa watu kama hao," alisema."

"Lakini kwa sababu siungi mkono hukumu ya kifo, nadhani tunahitaji kuongeza hukumu kuwa  kifungo cha maisha kwa watu kama hao,"

Mbunge huyo wa ODM alitaka viongozi wengine Bungeni kuunga mkono muswada wa adhabu kali kwa washukiwa wa vitendo hivyo.

Alisema kkuwa watu wanapaswa kuzingatia madhara ya vitendo vyao kabla ya kuchukua hatua ya kusambaza picha kama hizo.

"Angalau kama hujali mhusika, wahurumie watoto wake," alisema.

Nchini Kenya, kusambaza picha za uchi ni hatia na inaweza kuadhibiwa kwa kifungo cha miaka miwili ama faini ya hadi shilingi  laki mbili.

Mapema wiki hii, video ya mwanamke aliye uchi iliyorekodiwa wakati usiojulikana ilisambazwa kwenye mitandao ya kijamii huku baadhi ya Wakenya wakidai mhusika ni CAS Omanga. Hata hivyo, hakuna kilichothibishwa kufikia sasa.

Siku ya Jumanne asubuhi, Waziri huyo msaidizi mteule katika wizara ya usalama wa ndani  alivunja kimya baada ya kile kinachodaiwa kuwa video yake ya utupu kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii.

Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Facebook, Omanga alinukuu Bilbia yenye kifungo cha kujiliwaza ambapo Mungu anawaambia waja wake kwamba amewapa nguvu na hakuna kitakachowaumiza.

“Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru." Luka 10:19. Siku njema wadau,” aliandika.