Omtata awasilisha kesi kumzuia Mwilu kuchukuwa nafasi ya Maraga

Muhtasari

• Omtatah anataka korti izuie  JSC kumteua Mwilu kuchukua nafasi ya Maraga.

• Omtatah anasema kesi hiyo ni ya dharura kwa sababu Maraga yuko tayari kwenda likizo ya kustaafu.

• Anashutumu JSC kwa kujikokota kuamua swala la Mwilu.

Jaji Mkuu David Maraga akishauriana na Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu na Jaji Smokin Wanjala wakati wa kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais, Novemba 14, 2017. Picha: JACK OWUOR
Jaji Mkuu David Maraga akishauriana na Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu na Jaji Smokin Wanjala wakati wa kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais, Novemba 14, 2017. Picha: JACK OWUOR

Mwanaharakati wa Haki za Binadamu Okiya Omtatah anasema Naibu Jaji mkuu Philomena Mwilu hafai kuhudumu katika wadhifa wa Jaji Mkuu wakati David Maraga anapostaafu Januari 2021.

Katika kesi iliyowasilishwa kortini, Omtatah anataka korti izuie Tume ya Huduma za Mahakama kumteua Mwilu kuchukua nafasi ya Maraga hadi pale ataondolewa madai ya ufisadi yanaomkabili.

"Tukisubiri kusikizwa kwa pande zote na uamuzi wa kesi hii, korti inatoa agizo la muda kuzuia JSC kumteua Mwilu kuchukua nafasi katika ofisi ya Jaji Mkuu, hadi pale tume itakapomwondoleo madai ya ufisadi na matumizi mabaya ya ofisi katika kesi nne zinazomkabili” Ombi hilo lilisema.

 

Omtatah anasema kesi hiyo ni ya dharura sana kwa sababu Maraga yuko tayari kwenda likizo yake ya mwisho kutoka Jumanne wiki ijayo na Mwilu anatarajiwa kushika wadhifa wa kaimu Jaji mkuu akisubiri uteuzi wa Jaji mkuu mpya.

Mwanaharakati huyo anaendelea kusema kuwa kwa sasa kuna maombi nne tofauti yaliowasilishwa kwa JSC kutaka Mwilu aondolewe afisini.

"Kwa mfano, DPP na DCI wanadai katika ombi lao kwamba Jaji Mwilu hafai kuhudumu katika  ofisi ya umma kwani alihusika katika uuzaji na ununuzi wa mali kwa njia isiyo ya kawaida ikiwa ni pamoja na kupata hakikisho kwa njia za uwongo," Omtatah anadai.

Omtatah anasema ana wasiwasi kwamba tume ambayo ina jukukumu la kuhakikisha kwamba hadhi ya majaji inazingatiwa, inachelewesha kwa makusudi kuamua swala la Mwilu.