IEBC yamruhusu Waititu kuwania ugavana wa Nairobi

Muhtasari

 • Waititu alifurushwa kutoka wadhifa wa gavana wa Kiambu na bunge la kaunti.

 • Alikuwa amezuiwa kuania wadhifa wowote wa umma na EACC kwa sababu za ufisadi.

 • Wadhifa huo ulibaki wazi baada ya Mike Sonko kufurushwa.

Aliyekuwa gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu
Aliyekuwa gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu

Aliyekuwa Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu amepata afueni katika azma yake ya kumrithi Mike Sonko kama Gavana wa Nairobi.

Hii ni baada ya tume ya uchaguzi na mipaka IEBC kuchapisha jina lake kati ya wagombeaji 12 huru wanaotaka kuwania ugavana wa Nairobi.

Waititu, maarufu kama Babayao hapo awali alikuwa amepinga uamuzi wa tume ya uchaguzi kumzuia kugombea katika uchaguzi mdogo wa gavana wa Nairobi.

 

Waititu alikuwa amekosea uamuzi wa IEBC akisema ingawa anakabiliwa na kesi ya ufisadi, hajahukumiwa kwa kosa lolote na kwa hivyo ana haki ya kuwania ugavana.

"Kama ilivyo sasa, mlalamishi katika suala hili hajahukumiwa kwa uhalifu wowote na amefuata kikamilifu miongozo yote ya uchaguzi iliyotolewa wakati wa kuwania nafasi hiyo ya uchaguzi iliyotajwa hapo awali," korti iliambiwa.

Waititu alishtakiwa akiwa gavana wa kaunti ya Kiambu mwaka 2020 lakini tangu hapo ameonyesha nia ya kugombea kiti cha kaunti ya Nairobi katika uchaguzi ujao, ambao umesimamishwa kusubiri kesi iliyowasilishwa na Sonko.

Wadhifa wa gavana wa Nairobi ulibaki wazi baada ya bunge la kaunti kupiga kura ya kutokuwa na imani na gavana Mike Sonko.

Taaluma ya kisiasa ya Waititu ilionekana kuchukua mwelekeo mbaya baada ya EACC kuonekana kumfungia nje kushikilia afisi yoyote ya umma.

Katika taarifa mwezi uliopita, EACC ilisema watu wote wanaojitolea kama wagombeaji huru au wanaotafuta uteuzi wa vyama kwa uchaguzi lazima wafikie kiwango cha uadilifu chini ya Sura ya 6 ya Katiba.

"Tume inamchukulia mtu kuwa hana haki ya kushika wadhifa wa umma ikiwa mtu huyo ameachishwa kazi au ameondolewa mamlakani kwa kukiuka Sura ya 6 ya Katiba au sheria yake, kwa mujibu wa kifungu cha 75 (3) cha Katiba," EACC ilisema.

 

Wagombea wengine huru ni pamoja na Ogwang Raymond Ndungu, Kiigi Evans Machoka, Lengala David William, Hassan Jimal Ibrahim, Dkt. Noah Winja, Otieno Aloys Lavern, Mukundi Mathenge, Munyanya Yassin, Olingo Timothy Ayieko na Njuru Phyllis Wangari.

Katika ilani hiyo hiyo, IEBC ilitangaza kuwa Dennis Waweru, Agnes Kagure, Betty Adhiambo, Alex Kipchirchir na Habib Omar watachuana chini ya mchujo wa Chama cha Jubilee uliopangwa Januari 9.

Uchaguzi mdogo wa ugavana ulikuwa umepangiwa kufanyika Februari 18, lakini Korti ilisitisha hadi ombi lililowasilishwa na Sonko lisikilizwe na kuamuliwa.